Sambaza....

Naaam!! Watu wamesadiki, watu wamekubali kuwa ligi yetu inakua. Ni wazi na ni kweli isiyopingika kuwa ligi yetu ni bora sasa, ni moja ya ligi kumi bora barani Afrika.

Tumeona na kushuhudia vilabu vikisaini mikataba mikubwa, mirefu na minono, hii ni ishara ya kukukua. Sajili kubwa za wachezaji kutoka pande zote za ulimwengu kwa vilabu vyetu ni ishara ya kukua kwetu.

 

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia limekuwa likifanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha shughuli za soka zinaendesha kikamilifu, isitoshe Shirikisho linapambana kutafuta wadhamini wengi zaidi ili kuidhamini ligi ya Tanzania.

Licha ya kazi hii kubwa lakini bado shirikisho linaingia mikataba migumu isiyo na vipengele vya kuhoji wala kutoa ushindani. Tarehe 11 mwezi huu TFF waliingia na kusaini makubaliano na benki ya NBC juu ya kuidhamini ligi kuu pamoja na Championship ( ligi daraja la kwanza) kwa makataba wa thamani ya billioni 32.

Hotuba ya rais wa Shirikisho katika hafla hiyo ilizua gumzo vichwani mwa watu na kuwaachia maswali magumu kiasi ya kushindwa kutapa majibu. Rais huyo alisema “Naomba nitoe karipio kali kwa vilabu na wachezaji ambao kwa namna moja au nyingine wanahujumu au watahujumu haki za mdhamini kwa kuwafaidisha washindani wake wakibiashara kwa maslahi binafsi.”

Rais wa TFF Wallace Karia.

Tumeona hivi karibuni vilabu vyetu kama vile Simba na Yanga vikiingia mikataba na benki za CRDB na NMB kama washirika wao binafsi. Sasa katazo hili na karipio kutoka TFF linakwenda kuwaumiza walaji wake ambao ni vilabu kwani wanaushirika na washindani wakibiashara ya mdhamini wa ligi ambaye ni NBC.

Hii inaenda mbali kiasi cha kuingilia hadi mambo binafsi ya wachezaji kwani wapo baadhi ya wachezaji wa ligi kuu Tanzania Bara wameingia makubaliano na benki za CRDB na NMB kuwatangaza na kuwa mabalozi wao. Hivyo kwa katazo hili wanakosa uhalali wa kuitumikia mikataba yao eti wakihusishwa kuwahujumu wadhamini wa kuu wa ligi ambao na NBC.

“TFF pamoja na bodi ya ligi hatutavumilia tena kuona haki za kimkataba za mdhamini zinakiukwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yoyote anayehusisha wapinzani wa kibiashara wa mdhamini kujinufaisha na Ligi kuu na ile ya Championship. Ni jukumu letu kulinda maslahi ya mdhamini, hatutavumilia tena migongano ya kimaslahi na ujanja wa aina yoyote katika soka la Tanzania na Ligi zetu,” aliongeza Rais Wallace Karia.

Viongozi wa Benki ya CRDB na Yanga Sc katika hafla ya kutia saini ya mashirikiano.

Swali la msingi, Je NBC wameidhamini Ligi Kuu au wamevidhamini vilabu vyote vya Ligi na Chmapionship? Je vipi kuhusu watu binafsi ambao ni wachezaji?

Ifike mahala Shirikisho la soka lijitathimini linapoingia mikataba ya udhamini, kama kweli hili tamko la TFF watalitilia maanani basi tutarajie kuona vilabu vyetu na wachezaji kufa masikini.

Wadhamini wengi zaidi ndio huvisaidia vilabu vyetu kuweza kumudu gharama za kuendesha shughuli zao, kupigwa marufuku na katazo kwa wadhamini wenza hususani kwa vilabu basi tunakwenda kuviteketeza vilabu vyetu na kuvifanya viendelee kutia huruma kujiendesha na kubwa zaidi ni kuwafanya wachezaji wasiione faida ya kucheza soka kwa kukosa haki za kuwa na wadhamini binafsi kisa tu wanakinzana kibiashara na wadhamini wa ligi.

NB: LETA KAMA TULIVYO.

Sambaza....