
Ukiachana na Marc Wilmots, Paul Van Himst, Benard Voorhoof anayefuata sio Edin Hazard wa Chelsea bali ni mtu mwenye miraba minne, anamiliki uzito wa kilo 94, na urefu wa 1.9m sawa na futi 6 na inchi 3, tangu mwaka 2010 hadi leo ameifungia timu yake ya taifa magoli 45 katika mechi 79 alizocheza na kuwa mfungaji bora wa muda wote.
Gharama za uhamisho wake kutoka Everton mwaka 2017 zilikuwa ni Euro milioni 85. Ukiachana na Neymar, Ronaldo, Mbappe na yeye yupo 10 bora kwa gharama kubwa za usajili. Huyu ndie Romelu Menama Lukaku Bolingoli.
Amechezea
vilabu vingi kabla ya kutua Old Traford. Alishawahi kukiwasha na Chelsea miaka
ya 2011-2014 lakini mwaka 2012 akiwa Chelsea alipelekwa kwa mkopo West Bromwich Albion, akicheza mechi 35
akifunga magoli 17, kisha akapelekwa kwa mkopo Everton mwaka 2013 kabla ya
kununuliwa jumla jumla mwaka 2014-2017 na hapo ndipo ufalme wa Lukaku
ukaonekana.
Ameifungia
Everton magoli 53, katika mechi 110 alizocheza, na hiki ndicho kilichomshawishi
Mreno Jose Mourinho kuona ni mtu sahihi kwa timu kubwa kama Manchester United,
na tayari ameshaichezea Man U mechi 60 na kuifungia magoli 28.
Katika ligi
kuu nchini Uingereza, EPL Lukaku tayari amesha weka kambani magoli 12 na
kumuweka nafasi sawa na Edin Hazard wa Chelsea, Raheem Sterling wa mana city na
Alexandre Lacazette wa Arsenal.
Lukaku ni
miongoni mwa wachezaji wa Man U wanaotamkwa sana midomoni mwa mashabiki na
wadau wa soka duniani, si kwa uzuri kama anavyosemwa Paul Pogba bali ni kwa
ubaya hasa wa kubeza kiwango chake, wengine wakisema amenenepa bila mpango. Kila
mtu ana lake la kusema.
Hivi majuzi
Man U ilimrarua Southampton na Lukaku alizisabahi nyavu za Southampton mara
mbili, mashabiki wa Man U walijawa na furaha na kusahau kuwa Lukaku ana kilo 94.
Lukaku
ameshacheza dakika 1694, amefunga magoli
12, sawa na goli 1 kwa kila dakika 141, sawa na mechi mbili kasoro dakika 39
mpira kumalizika. Na amepiga mashuti 38,
asilimia 74 ya mashuti yake yamelenga
lango.
Tafsiri ya
takwimu hizi ni kwamba, Lukaku amefunga magoli 12 pekee katika nafasi 38
alizopata za kupiga shuti. Wastani wa ufungaji wake ni sawa na kucheza mechi
moja na dakika 51. Kumbe ndio maana
tunamlaumu, tunambeza na bado akifunga tunamsifu hii ni dalili kuwa tunamtegemea.
Masikini JOHN
BOCCO naye kaingia kwenye mtego sawa na
wa Lukaku. Au sijui kwa sababu wote ni WEKUNDU! Bocco naye anasemwa sanaa, tena
na mashabiki wa timu yake na hata upande wa pili. Wengi wanasema ameshachoka,
akipata nafasi 6 za wazi anatumia 2 lakini akifunga utasikia tu” huyo ndio PAPA
JOHN BOCCO” yaani huitwa majina yote ya kumsifia.
Kwa mwezi
Februari pekee Bocco amefunga goli 4 sawa na Salimu Aiyee wa Mwadui fc,
amewapiga “gap” Ayubu Lyanga wa Coastal na Salumu Mashaka Kimenya wa Prisons
wenye goli 2 na 1 mtawalia. Lakini amepitwa na Meddie Kagere mwenye goli 5.
Nani
asiyejua kama Bocco ndiye aliyetoa pasi ya goli la Meddie Kagere dhidi ya
Mwarabu Al-Ahly uwanja wa taifa? Vipi dhidi ya mahasimu wao Yanga? Alitoa pasi
ya mwisho pia. Hakuishia hapo , mechi iliyofuata alifunga magoli mawili dhidi
ya African Lyon kule Arusha.
Dhidi ya
Azam alifunga goli, katika ushindi wa 3-1. Dhidi ya Stendi United tena anafunga
goli 2. Kwa mantiki hiyo Bocco amehusika matika mechi 5 mfululizo. Lakini bado
anabezwa, si na mashabiki wa upande wa pili na hata mashabiki wa Simba.
Ukiachana na
hayo yote, Bocco ana rekodi nyingi zinazombeba kuwa mchezaji mkubwa. Idadi
kubwa ya magoli ligi kuu Tanzania bara anayo yeye, yeye ndiye mfungaji bora wa
muda wote, anagoli zaidi ya 100. Mchezaji aliyezifunga goli nyingi timu za
Simba na Yanga rekodi pia anayo yeye. Ni mchezaji bora wa msimu uliopita. Na ni
kepteni wa timu kubwa kama Simba. Bado unamchukulia
poa tu?.
Mara zote
amekuwa akikiri kukosa mabao mengi tu awapo uwanjani, mfano ni mechi dhidi ya
Mwadui, alikosa nafasi 3 za wazi. Kushindwa kubadili nafasi kuwa goli ni sehemu
ya sifa ya Straika, kuna wakati anakosa na kuna wakati anazitumia hata zile unazoziona sio nafasi za
goli, mfano ni goli alilofunga dhidi ya Prinsons kule Mbeya msimu uliopita. Alifanya
“fantastic turn” na kufunga bao la kideo.
Ni huyu huyu
Bocco mfalme wa Azam wa muda wote, timu ilianzia mikononi mwake, na hata baada ya
yeye kuondoka akiwa na marafiki zake Shomari Kapombe, Aishi manula na Erasto Nyoni
Azam nayo imeisha makali yake, sio Azam ile ya John bocco na Joseph Omog.
Kiufundi Bocco hufanya nini uwanjani?
Mechi tano
za hivi karibuni kama hajafunga basi atakuwa ametoa pasi ya goli. Unadhani
kwanini Bocco akiwa fiti huwa haanzii benchi ukilinganisha na Kagere na Emmanuel
Okwi? Bocco ni mpambanaji, ni kiongozi ndani ya uwanja . Thamani ya yeye kucheza
hata asipo funga ni kubwa.
Bocco
huhitaji nafasi ndogo kupiga shuti, mipira ya juu yote ni uhakika kuchezwa na
kichwa cha Bocco. Hii inatoa uwanda mpana kwa timu kushambulia chini na juu kwa
wakati mmoja. Bocco ni mkabaji, hukaba kuanzia eneo la juu la timu pinzani. Timu
ikizidiwa eneo la kati itakuwa na uwezo wa kupiga mipira mirefu ya juu kwa
sababu yupo mpokeaji wa mipira hiyo. Kimo kinamuunga mkono.
Bocco hukaa
juu kama straika wa pembeni ya Kagere, yaani Bocco humzunguuka Kagere muda wote
akihaha kushuka chini kulia na kushoto kupokea mipira, huku Kagere akibaki kama
straika wa mwisho, ili asiliache eneo la mabeki wa kati wazi, asiwafanye watoke
kwenda kushambulia.
Bocco
humsaidia Kagere kubaki eneo la juu, na kuwafanya mabeki wasipandishe timu.Bila
Bocco, Kagere angekuwa anahaha kushoto na kulia na matokeo yake eneo la mabeki
wa kati wa timu pinzani linakuwa halina hatari yoyote. Na hiki ndicho
kilichotokea dhidi ya AS Club Vita, athari yake ni Simba kula tano.
Hadi kufikia
hapa bado unambeza tu Bocco? Huenda ulikuwa humjui vizuri anafanya nini nje na
ndani ya uwanja, huenda ulikuwa hujui rekodi zake, huenda ulikuwa hujui ukubwa
wa Bocco nje ya Simba. Sasa utakuwa unajua, bado utamchukulia poa tu Bocco?
Umesahau penati yake dhidi ya Nkana, Kitwe Zambia ilizaa goli lililoipa ahueni
Simba ya kushinda uwanja wa taifa?
Lukaku na
Bocco hawa ndio wapo tayari kutoa jasho na damu zao kwa ajili ya timu zao ndio maana hata hawashughulishwi na kusemwa
na mashabiki wala vyombo vya habari. Kiukweli “ tunawabeza machoni lakini
tunawategemea mioyoni”.