Sambaza....

Macho yangu yashawahi kufunuliwa ulimwengu wa Frank Lampard na Cesc Fabregas, ulimwengu ambao ni nadra sana kuuona kwa sasa. Siyo mara nyingi sana kukutana na ulimwengu huu wa kufurahisha.

Ulimwengu ambao Frank Lampard umemfanya awe mfungaji bora wa wakati wote wa klabu ya Chelsea. Huyu hakuwahi hata kuwa mshambuliaji wa kati. Miguu yake ilikuwa inatokea katikati ya uwanja, lakini roho yake ilikuwa inaishi karibu sana na nyavu za magoli.

Akili yake muda mwingi ilikuwa inawaza namna ya kudumisha ndoa yake na nyavu, ndoa ambayo aliipenda sana na cha kufurahisha hata nyavu zilimpenda sana kwa pamoja wakajenga mahusiano yaliyokuwa yanatufurahisha sisi ambao tulikuwa tunashuhudia harusi yao.

Harusi yao ilisindikizwa na mafataki ya kila aina, kuna mafataki ambayo Frank Lampard alikuwa anayaachia akiwa nje ya kumi na nane na kuna mengine ambayo alikuwa anayaachia ndani ya kumi na nane, yote haya aliyafanya kumfurahisha msichana anayeitwa nyavu.

Hakutamani sana kumuona msichana anayeitwa nyavu akiwa amejenga taswira ya kununa katika uso wake. Hakutegea kabisa alikuwa kwenye ujenzi wa tabasamu, hata kipindi ambacho kina Didier Drogba walishindwa kutengeneza tabasamu kwenye uso wa nyavu yeye alikuja kukamilisha kazi.

Ndiyo maana hutoshangaa hata kurasa za historia za ligi kuu ya England zikituambia Frank Lampard kamaliza maisha yake ya soka akiwa na magoli 177 katika ligi kuu ya England na huyu akiwa kiungo wa katikati ya uwanja.

Hata Baada ya yeye kuondoka Chelsea alikuja Cesc Fabregas , naye alikuwa na sifa hizo hizo za Frank Lampard. Anafunga na anatoa pasi nyingi za magoli. Kuna kipindi timu zinapokuwa zimeshindwa kupata magoli , washambuliaji wameshindwa kuzifurahisha nyavu, Frank Lampard au Cesc Fabregas walikuwa ni suluhisho.

Hiki kitu hakipo kwetu , hatuna Frank Lampard wetu au Cesc Fabregas wa kujivunia. Viungo wetu wa Kati siyo wafungaji sana. Wanafunga mara moja moja sana. Sawa Jana SureBoy alifunga goli la ushindi. Hii hutokea mara chache sana, kuna wakati timu yetu hubanwa sana hasa hasa washambuliaji wetu lakini kwa bahati Mbaya mara nyingi hakuna kiungo ambaye huibuka kama shika.

Sambaza....