Kuna muda tulitumia muda mwingi sana kumwandika, mikono yetu ilikuwa inatoa tabasamu kila tulipokuwa tunamwandika Ibrahim Ajib.
Hata midomo yetu ilikuwa na furaha kubwa sana kila tulipokuwa tunamtaja Ibrahim Ajib. Midomo yetu ilikuwa inaona fahari kumtamka.
Tena tulitumia muda mwingi sana kumtafutia majina ya kuvutia kupitia midomo yetu. Yupo aliyesema kuwa Ibrahim Ajib ni fundi.
Kuna mwingine alidiriki kusema kuwa ni mchezaji wa ajabu tena wa kipekee aliyeshushwa na mwenyezi Mungu.
Mungu hakutumia muda wake kwa ajili ya kumuumba, ila aliamua kumshusha tu dunia ili aje tu afanye kazi moja tu, nayo ni kutoa burudani kwa watu kwa kutumia miguu yake.
Miguu ya dhahabu, miguu yenye kila aina ya burudani. Miguu ambayo ina hadhi kubwa kuzidi ligi ambayo anacheza Ibrahim Ajib.
Ndiyo maana kuna wakati tulimpigia kelele sana atoke hapa nchini aende sehemu ambayo ilikuwa ndiyo hadhi yake.
Tulimfukuza kwa nia nzuri tu, kumfukuza kwetu hakukuwa tunamaanisha kuwa tulikuwa tunamchukia.
Tulikuwa tuɓamfukuza kwa mazuri. Hatukutaka kabisa kumuona akiishia kucheza hapa. Hatukutaka kumuona akimaliza soka akiwa masikini.
Tulitamani kuona tukitengeneza vijana wengi matajiri kupitia mpira, tulitamani kuona timu yetu ya taifa ikiwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza ligi ya nje.
Tulitamani kuona Ibrahim Ajib akicheza katika ligi kubwa barani ulaya. Tulitamani kabisa kumshuhudia akitoa pasi za mwisho nyingi za magoli akiwa kwenye michuano ya klabu bingwa barani ulaya.
Tuliamini kuwa anaweza kufanya hivo kwa sababu tu ana kipaji kikubwa ambacho tulikuwa tunakishuhudia kila akikanyaga nyasi za ligi kuu yetu.
Nyasi mbovu, nyasi ambazo hazina afya, nyasi ambazo Ibrahim Ajib hakutakiwa kabisa kuzitumia kwa ajili ya kucheza hii ligi.
Kelele zetu zilikuwa nyingi sana kipindi hicho, kila mtu alitamani Ibrahim Ajib asikie matamanio yetu ili tu aende sehemu ambayo ni bora.
Lakini kadri siku zinavyozidi kwenda kelele zetu zimepungua sana , pamoja na kwamba kelele zetu kupungua lakini kiwango cha Ibrahim Ajib kipo pale pale.
Watu hawakioni?, kama wanakiona kwanini hawaendelei kuimba ule wimbo wa kunfukuza Ibrahim Ajib?
Nahisi tumeanza kuchoka kuongea, tushaanza kuzoea kiwango cha Ibrahim Ajib na kila anachokifanƴa kwa sasa tunakiona cha kawaida kwa sababu ashawahi kukifanya huko nyuma.
Hakuna cha ajabu ambacho anachokifanya kwa sasa kwa sababu anafanya marudio. Hakuna jipya, ndiyo maana watu wako kama hawamuoni.
Na taratibu washamsahau na wamechoka kuendelea kuona vitu ambavyo ni vile vile. Kuna kitu kimoja kipya tu ambacho anatakiwa kukifanya kwa sasa.
Ni yeye kuondoka hapa. Hiki ndicho kitu pekee ambacho hajawahi kukifanya. Na ndicho kitu ambacho wengi tunakisubiri. Na ndicho kitu ambacho kitatufanya tuanze kumuongea sana.
Sasa hivi tumepunguza kumuongea sana kwa sababu anafanya marudio ya vitu ambavyo tushaviona akivifanya. Anachotakiwa kukifanya ni kimoja tu. Kufanya kitu kipya ambacho hajawahi kukifanya, aache kuipa adhabu miguu yake kwa kuiweka kwenye viwanja vyetu vibovu.