Mengi ya maswali huwa ni magumu kupata jibu lake kipindi ambapo unapokosa kipaumbele katika maisha yako, ndiyo maana hata nilipokuwa mtoto mdogo nilikosa jibu zuri la kumpa baba aliponiuliza kipi ninapenda kati ya somo la hesabu au kuhesabu pesa zangu.
Kichwa kilikuwa kizito kutoa jibu la moja kwa moja kwa sababu sikuwa najua kipaumbele changu kikubwa kwenye maisha yangu.
Kipi nilikuwa nakitaka kwa dhati kwenye maisha yangu?, kwa kifupi ipi ilikuwa ndoto yangu?, na kipi nilichokuwa kuwa natakiwa kukifanya ili ndoto yangu itimie?.
Haya ndiyo maswali makubwa mazito na yenye umuhimu mkubwa sana kipindi ambacho umeshajua kipaumbele chako kufikia maono yako.
Na huu ndiyo mtihani mgumu ambao mtu binafsi, taasisi na makampuni mengi yasiyo na maono makubwa hushindwa kuujibu na hii ni kwa sababu hawana kipaumbele, hawana maono kwenye kitu ambacho wanakifanya na ndiyo maana ni rahisi kukuta hawana maendeleo makubwa kulingana na umri wao kwenye kazi husika.
Umri wetu ni mkubwa sana kwenye ngazi ya michezo lakini maendeleo yetu yamekuwa butu kwa sababu tumekosa maono, maono ambayo yanaweza kutuongoza kupata kipaumbele cha kipi ambacho tunatakiwa kuanza nacho.
Na ndiyo maana tunapenda kutengeneza matukio ya muda mfupi ili tuonekane tunafanya kazi vizuri, tujisifu na tusifiwe kutokana na tukio la muda mfupi ambalo tunalipanga kwa ajili ya kuteka macho na masikio ya watu kwa muda mfupi.
Lakini baada ya hapo tukio hilo la muda huisha na sisi kurudi kwenye uhalisia wetu, uhalisia ambao unatuonesha michezo ni sehemu ya kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya na siyo sehemu ya ajira.
Ninajua kabisa baada ya leo Rais John Pombe Magufuli kukabidhi hili kombe kitu ambacho tutabaki nacho kwenye vinywa vyetu ni kuwa Simba ni timu ya kwanza kukabidhiwa kombe la ubingwa na Rais bila kufikiria kitu hicho kina afya kwenye sekta hii ya michezo?
Simaanishi kwamba kualikwa kwa Rais kuikabidhi Simba kombe la ubingwa ni kitu kibaya, maana yangu ni moja tu hiki ndicho kipaumbele chetu kufikia maono yetu?, ni kipi kitafuata baada ya Rais kukabidhi kombe hili ? , tutaishia kumfurahisha kwa nyama tuliyompikia bila kumwambia shida tunazopata wakulima? , tutaishia kujitapa na kujisifu kisa Rais katukabidhi kombe hili?.
Hapa ndipo ninapokuja kuona kuwa hili ni tukio la muda ambalo limepangwa kwa ajili ya kujipa furaha ya muda tu na hii ni kwa sababu nchi yetu inapenda kuongozwa kwa matukio tu kila sehemu.
Ningefurahia zaidi kama kiwanda hiki cha michezo kingekaa na raisi ili kujadiliana mambo yenye afya ya baadaye katika michezo. Tuna vingi vinahitajika ili kuimarisha afya yetu katika michezo.
Rais wetu amekuwa akihimiza kuhusu”Tanzania ya viwanda” na moja ya kiwanda ambacho kinatoa ajira kubwa sana kwa vijana, ajira ambayo ina chanzo kikubwa cha pesa lakini kiwanda hiki akiangaliwi kama sehemu rasmi.
Ningefurahia viongozi wanaoongoza kiwanda hiki cha michezo wangeomba kukutana na raisi ili wamshauri namna ambavyo anaweza kubadili sera ya taifa ya michezo ili iitambue michezo kama sekta rasmi.
Wangemuonesha namna ambavyo michezo inasaidia kuingiza pato la Taifa kupitia kodi na ajira ambazo watu mbalimbali hupata kupitia michezo.
Hii ingekuwa mwanzo wetu wa kuitambua sekta hii kama sekta rasmi hata mwamko wa chama cha mapinduzi kukarabati miundombinu yake ya michezo ( viwanja vyake) ungekuwa mkubwa kwa sababu Rais John Pombe Magufuli ndiye mwenyekiti wa chama hiki.
Angeona ni wakati sahihi kwake yeye kukarabati miundonbinu ya viwanja hivi ili viendane na mazingira ya sasa ya kibiashara.
Biashara hii ya michezo huanzia chini, chini ambapo vipaji mbalimbali huibuliwa, tuna tatizo kwenye hili. Hatuna mfumo rafiki wa sisi kuibua vipaji, kuvilea na kuviendelezea ili vikue katika mazingira mazuri ambayo yatakuwa na manufaa kwenye
taifa letu.
Huu ndiyo ungekuwa wakati mzuri kwetu sisi kumshawishi mkuu wa nchi kuanzisha shule maalumu ya michezo kwa kila kanda. Kila kanda kungekuwa na shule maalumu kwa kuibua vipaji , kuvilea ili vije kutumika kwa manufaa ya taifa letu.
Hii ingetoa fursa ya kuwa na wachezaji wengi wenye elimu kama ilivyo kwenye nchi ya Ubelgiji.Wao walifanikiwa kwenye mpira wa miguu kwa kutumia taasisi za elimu.
Tunatamani sana kila siku wachezaji wetu kucheza katika nchi za nje ili tupate timu ya taifa imara lakini hatuna njia nyingi za kuwafanya wachezaji wetu wafike huko tunakopatamani.
Huu ndiyo ulikuwa wakati mzuri kwa viongozi wa viwanda vya michezo nchini kumshauri raisi ashauriane na nchi mbalimbali zilizoendelea katika michezo mbalimbali ili tupeleke watoto wetu wenye vipaji katika shule na vituo vyao vya kulelea vipaji ili wakue katika misingi bora.
Lakini hivi vyote tumesahau na akili zetu zimetuaminisha katika tukio la muda mfupi wakati hata sheria za uendeshaji wa vilabu vyetu hivi vya wanachama haviruhusu kwa asilimia kubwa kuendeshwa kisasa.