Mashabiki wa soka wa Tanzania wamekua na muamko sana, wamekua wakizifuatilia na kuwa karibu na timu zao.
Timu zinajiingizia vipato kutokana na vyanzo mbalimbali kama vile makusanyo ya getini, haki za matangazo, wadhamini na mauzo ya jezi. Haki za matangazo, wadhamini na viingilio vimekua muhimili wa uchumi wa vilabu vyetu kwa muda mrefu sasa, na suala la uuzaji jezi na vifaa vya michezo limeshika kasi katika miaka ya hivi karibuni.
Ubunifu, weledi na uwekezaji katika sekta ya uzalishaji jezi umekuja kuibua chachu na hamasa ya mashabiki kujenga uchumi wa vilabu vyao pendwa kwa kununua jezi. Mikataba minono na mikubwa tunaona ikisainiwa na vilabu vya ligi kuu Tanzania bara kwa ajili ya uzalishaji wa jezi na vifaa vya michezo.
Inapendeza sana kuona mashabiki wamevalia jezi za timu zao na kwenda uwanjani, Licha ya muamko na uwekezaji mkubwa katika uzalishaji jezi lakini upatikanaji wake bado umekua mgumu na wamateso, mashabiki wanapata kadhia na usumbufu katika kupata jezi za timu zao, jezi zimekua zikichelewa kupatikana sokoni inafikia pahala msimu mpya unaanza angali jezi mpya za msimu husika hazijatoka mfano msimu uliopita kuna baadhi ya timu zilianza msimu na jezi zisizo rasmi na nyingine za msimu ulokwisha, mfano Kagera Sugar Vs Namungo mchezo wa kwanza pale Nangwanda sijaona Mtwara,.
Jezi zimekuwa zikiletwa kimafungu na kwa mgao kiasi cha kushindwa kutimiza haja na kukata kiu ya mashabiki na katika uchache huo zinapatikana kwa gharama kubwa zaidi ya ile iliyopangwa na vilabu na hii inatokana na uchache wake sokoni.
Nini kiko nyuma ya hili? Kipi kifanyike kutatua hili? Shabiki anaweza kujiuliza maswali haya pengine akakosa majibu lakini kuna mambo mengi nyuma ya hili mfano:
• Ufuatiliaji mdogo wa viongozi na mahusiano mabovu na kampuni zinasohusika; ni kama viongozi hawawajibiki ipasavyo kwani msukumo na ufuatiliaji ni mdogo kiasi kwamba wazalishaji wa jezi hufanya kazi wapendavyo bila kujali muda wa kupeleka bidhaa sokoni na kuwapa thamani walaji. Viongozi wanatakiwa wawajibike ipasavyo wafanye kazi kwa ukaribu na wazalishaji ili kujua changamoto zao na kuhakikisha bidhaa inawafikia walaji (mashabiki) kwa wakati mfano timu za Ulaya huwa na utaratibu wa kutambulisha jezi mpya mwishoni mwa msimu kabla ya msimu mpya kuanza na hii inachagizwa na ufuatiliaji na mahusiano mazuri na ya karibu kati ya viongozi wa vilabu na wazalishaji.
•Mikataba dhaifu; vilabu vyetu vingi havina ukwasi hivyo haviwezi kujitegemea vyenyewe kiasi kwamba vinalazimika kuingia mikataba yenye masharti magumu ambayo yanampa mzalishaji kufanya kazi atakavyo na sio kwa muongozo wa vilabu. Kwahiyo vilabu vyetu vinaposaini mikataba hii ya uzalishaji jezi waipitie upya na kwa umakini ili kuepuka mikataba kandamizi ambayo itawanyima haki ya kuhoji.
NB: KUKU ANAYETAGA HACHINJWI AKICHINJWA MSIBA.