Sambaza....

Klabu ya Tottenham Hotspur imezidi kupata pigo baada ya kuripotiwa kuwa kiungo raia wa Kenya Victor Wanyama anaweza kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kidogo kutokana na kuumia msuli wa paja wakati akiitumikia timu yake ya Taifa.

Wanyama ambaye aliiongoza Kenya hapo jana kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ethiopia katika mchezo wa kutafuta tiketi ya kushiriki Michuano ya Mataifa Afrika Mwakani, huku yeye akifunga bao la tatu kwa penati alifanyiwa mabadiliko kutokana na kuumia mguu.

Wanyama sasa anaungana na Jan Vertonghen ambaye ambaye atakuwa nje ya uwanja hadi mwezi Disemba akiwa na tatizo kama la Wanyama huku Dele Alli naye akiwa majeruhi toka katika mchezo wa Carabao Cup dhidi ya Watford.

Ikumbukwe kwamba msimu huu Wanyama ndo kwanza alikuwa anaanza kurejea uwanjani taratibu baada ya kuwa na majeraha ya muda ambapo mpaka sasa amecheza michezo mitano tu msimu huu akiwa na Tottenham na janga hili linamtokea.

Taarifa zinasema kuwa klabu hiyo inampango wa kumfanyia uchunguzi zaidi atakaporejea London kujua kama tatizo lake litachukua muda mrefu, hata hivyo anaweza kuukosa mchezo wa Jumamosi dhidi ya West Ham United.

Hata hivyo taarifa inaweza isiwe mbaya sana kwa kocha Mauricio Pochettino ambaye anatarajia wachezaji wake Mousa Dembele na Christian Eriksen kuanza kurejea uwanjani kuongeza nguvu baada ya kuwa nje kutokana na majeraha.

Sambaza....