Unaikumbuka ile timu ambayo ilifungwa mabao 20-0 mwishoni mwa juma hili kule nchini Italia? Basi imeondolewa kwenye ligi.
Timu hiyo kwa jina la Pro Piacenza imeondolewa kwenye ligi baada ya kubainika imechezesha wachezaji saba pekee kwenye mchezo huo ambao walifungwa na timu ya Cuneo katika ligi daraja la tatu nchini Italia (Italian Third Division).
Katika mchezo huo Pro Piacenza walichezesha wachezaji saba pekee na wachezaji wote walikuwa wenye umri chini ya miaka 18, huku nahodha wao Nicola Cirigliano mwenye umri wa miaka 18 pia alikuwa ndiye kocha katika mchezo huo.
Hata hivyo kabla ya mchezo huo wa Jumapili walishindwa pia kuhudhuria michezo mitatu mfululizo ya ligi hiyo.
Timu hiyo ambayo ipo katika matatizo makubwa ya kiuchumi ipo nafasi ya mwisho katika msimamo wa Kundi A la ligi hiyo, huku ikishindwa kabisa kuwalipa wachezaji wake hali iliyowafanya kuikimbia klabu hiyo.
Katika mchezo wa Jumapili ilibidi kuingiza uwanjani wachezaji saba pekee baada ya wachezaji wengine nane kusahau leseni zao, huku daktari wa timu baadae aliingia kama mchezaji wa akiba.
Sasa jana Jumatatu bodi ya ligi ilisema kuwa wachezaji wengine waliocheza mechi hiyo hawakuwa wamesajiliwa na hivyo kuwalazimu kuiondoa timu hiyo kushiriki ligi hiyo na kuipa ushindi Cuneo wa mabao 3-0.
Mbali na hilo pia Bodi ya ligi imeitoza faini timu hiyo ya Paundi 17,500 na kukiita kitendo kilichofanywa na timu hiyo kama kisichokubalika, kibaya na cha hatari kwa soka la Italy.