WAKATI ligi kuu Tanzania Bara ikiwa katika mzunguko wake wa tatu Shirikisho la soka nchini- TFF limetoa ‘kauli’ ya kushangaza kupitia rais wake Wallace Karia. Ikiwa ni mwaka mmoja sasa tangu angie madarakani Karia amesema hadi sasa TFF haijui bingwa na washindi wengine wa ligi hio watapata zawadi gani.
Hawajui! Bingwa atapata zawadi gani, mshindi wa pili hadi watatu, timu yenye nidhamu, mfungaji bora, mchezaji bora na zawadi nyingine ambazo kwa miaka zaidi ya 16 ya udhamini wa Vodacom Tanzania walikuwa wakizawadiwa kutokana na matokeo yao mazuri kwa miezi kumi ya msimu.
Ni maajabu kwa kweli kwa maana hata katika ligi za mitaani ‘Ndondo’ hata kabla ya kuanza kwa mashindano husika timu hufahamu ni nini ambacho wanaweza kushinda. Zawadi ndiyo kichocheo cha ushindani katika michuano/ligi yoyote ile na kwa hadhi ya ligi kuu ni jambo la kusikitisha/kushangaza mno kuona klabu zinacheza pasipo kujua nini ambacho wanaweza kushinda mwishoni mwa msimu.
KLABU ZINAPASWA KUGOMA.
Mwanzo wa yote ukiachana na kumalizika kwa mkataba wa udhamini Vodacom sababu kubwa iliyopelekea ligi kuu msimu huu kukosa mdhamini rasmi ni ongezeko la timu ambalo Karia amelifanya. Awali wakati Vodacom wanadhamini ligi hiyo ilikuwa na timu 20 mwaka 2002, baadae zikapunguzwa na kufikia timu 16 kufikia mwaka 2007 ligi kuu Bara ilikuwa na timu 12.
Zikapandishwa tena hadi kufikia timu 14, na kwa misimu minne iliyopita ligi kuu ilikuwa na timu 16. Kutoka timu hizo 16 hadi 20 msimu huu mkanganyiko ukaanza na Vodacom kama wadhamini walikuwa tayari kuboresha mkataba wao na Shirikisho lakini hawakuridhika na namna TFF ilivyoongeza timu kufikia 20.
Wao ( Vodacom) walitaka angalau ligi iwe na timu 16 lakini Karia na uongozi wake wakang’ang’ani na kusisitiza lazima ligi iwe na timu 20. Vodacom hawakuwa tayari kwa hilo wakajiondoa zao na wakati tukisubiri labda atapatikana mdhamini mpya, ligi ikaanza na juzi Karia amesema licha ya ligi kuendelea kuchezwa wao kama Shirikisho hawajui ni nini ambacho watazipa klabu na washindi wa ligi hiyo mwishoni mwa msimu.
Kwa mtazamo wa kimpira jambo hili ni tatizo na umefika wakati wa klabu kuungana kwa umoja wenye kuhitaji usawa kugomea kucheza ligi hiyo hadi pale watakapoambia nini wanachoshindania na washindi watapata nini. Kuendelea kucheza bila kufahamu ambacho kitatolewa ni makosa kwa sababu wanaweza kupewa zawadi ambazo hazistahili.
Labda mshindi wa kwanza atashinda kikombe, jezi na mpira na washindi wengine wakapewa labda jezi na mpira pekee hii inamaana kuwa TFF hawajui nini ambacho wanakifanya. Haiwezekani hata katika michuano ya mitaani timu kushinda pasipo kufahamu nini ambacho wanaweza kushinda.
Klabu zinapaswa zigomee kuendelea kucheza hadi pale Shirikisho litakaposema nini washindi watapa siku ligi ikimalizika ili kuondoa dhana ya kupewa zawazi yoyote tu ambayo itatolewa na TFF. Naamini kufanya hivyo ni haki yao kama klabu kwasababu huwezi kucheza pasipo kujua nini unatafuta.
Na ni wazi ni mwanzo tu wa kuelekea kushindwa kwa utawala wa Karia. Klabu ziamke usingizini sasa na waunane kujua watapewa jezi, ng’ombe, au katoni za juisi mwisho wa msimu kama zawadi za washindi. Nasisitiza klabu zinapaswa kuungana na kugomea ligi hii hadi pale watakapoambiwa nini watapata kama zawadi za washindi, au waambiwe tu zaidi ya vikombe na tuzo hakutakuwa na kingine chochote watakachopata.