Shirikisho la kandanda nchini (TFF) limeikana sauti inayosambazwa mitandaoni akisikika Rais Wallace Karia akitangaza kufungiwa kwa mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa Klabu ya Simba Haji Sunday Manara.
Taarifa ya TFF iliyosainiwa na Afisa habari Clifford Mario Ndimbo imesema sauti hiyo sio ya Rais Karia na yote ambayo yamesemwa katika sauti hiyo ni ya uongo yenye lengo la kupotosa na kuchafua taswira ya Taasisi ambayo ina utaratibu wake mzuri wa kutoa taarifa mbalimbali.
“Kumekuwa na sauti ya uongo inasambaa mitandaoni ikimuhusisha Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Wallace Karia akitangaza kufungiwa kwa Afisa habari wa klabu ya Simba Haji Manara, Sauti hiyo sio saui ya Rais wa TFF Ndugu Karia na maamuzi yaliyosemwa kupitia sauti hiyo ni ya uongo yenye lengo la upotoshaji na kuchafuia taswira ya Taasisi,” Imesema sehemu ya Taarifa hiyo.
Mwisho TFF imeendelea kuwaonya wale wote ambao wanatumia vibaya jina la Rais wa TFF kuacha mara moja tabia hiyo kwani ni kinyume cha sheria za mtandao, lakini pia kwa wale wanaondelea kuisambaza pia wamekumbushwa kuwa hiyo ni sehemu ya uvunjifu wa sheria za Jahmhuri ya Muungano wa Tanzania.