Kipindi hiki kila nchi barani Afrika, Asia, America na Ulaya kote nyasi zinapambana na mikimikiki ya mashindano ya ligi mbalimbali, mashindano ya vilabu bingwa na mechi za kimataifa kila timu fikra, mawazo, mbinu mbadala za uchezaji na za kiutendaji zinafikiria wanafanyaje kufikia malengo yao makuu.
Inashangaza kuona utaratibu huu kwetu unakuwa na mabadiliko kila kukicha kwa ratiba zetu kutokuwa madhubuti kutambuka changamoto za wakati na mapendekezo mbalimbali ya wadau na sasa limeenda mbali zaidi, tunajua wote kuwa samaki anayefumba mdomo wake hashikwi na ndoano ya mvuvi.
Kumbuka wewe TFF ndio kichwa cha familia hii ya vilabu vya soka, wachezaji, viongozi na mashabiki wa mpira wa miguu. Kumbuka wewe TFF ndio muhimili pekee wa kusimamia masuala mazima ya mpira wa miguu nchini kwetu Tanzania. Kumbuka wewe TFF ndio mlinda maslahi ya vilabu vya mpira wa miguu kwa kusimamia kiuhakika masuala ya utendaji na uendashwaji katika tasnia hii nchini kwetu Tanzania. Kumbuka wewe TFF ndio nguzo pekee inayoweza kutoa misimamo na dira zenye maono ya mbeleni na sio hizi za muda mfupi ambazo huwa hazina tija kubwa katika kuliendeleza soka letu nchini.
Kutoa baraka kwa mdhamini wa vilabu hivi na kuruhusu vilabu hivyo vishiriki katika bonanza hili lenye jina la Sportpesa halijaangalia maslahi mapana ya vilabu hivi wakati huu vilabu hivi wanaokabiliwa na mashindano ya ligi kuu na Klabu kama Simba ikiwa bado ni muwakilishi pekee katika mashindano ya klabu bingwa barani Afrika.
Nafasi pekee za uwakilishi wa timu yeyote katika mashindano ya nje, hapa kwetu Tanzania ni kupitia mashindano mawili tu LIGI KUU na AZAM FA Cup, ambayo mshindi wa kwanza hupata nafasi ya kushiriki mashindano ya Klabu bingwa barani Afrika na Kombe la shirikisho.
Sasa unapoona kipindi kama hiki kuna mashindano yeyote yasiyo na mlengwa huu yanafanyika nchini, sisi wapenda soka hushtushwa kidogo. Tukiangalia nafasi ya uwakilishi ya timu yetu ya Simba katika klabu bingwa bado kuna kazi yakufanya na jitihada zinahitajika ili kuweza kufuzu katika hatua hii waliyopo.
Hakuna kitu ambacho benchi la ufundi hawataki kukisikia kama wachezaji wao kupata majeruhi katika kipindi hiki, uwepo wa bonanza kama hili ambalo linashirikisha vilabu bora pia vya nchini Kenya inahitaji uwe na timu kamilifu itakayoshiriki vyema ili kuendeleza kuinua morali ya timu na mashabiki wake. Tumeona mfano mzuri mchezaji Erasto Nyoni alivyoenda kuumia katika kombe la Mapinduzi, kwa Simba wamepoteza very experienced player ambae angekuwa na mchango mkubwa sana katika mashindano haya na hatua hii ambayo Simba wamefikia ya makundi ya Klabu bingwa barani Afrika.
Tuache Maneno ya uwani, hatuombei mabaya kwa kusema wachezaji kushiriki kwao wanaweza wakaumia lahasha! Bali unawaweka katika nafasi hii ya uwezekano wa kuumia kwani ikumbukwe nafasi ya mshindi wa bonanza hili kuja kukutana na timu shiriki kombe la ligi kuu nchini Uingereza Everton si nafasi ambayo Klabu chochote kinaweza kuifanyia mzaha kwani ni moja ya nafasi nzuri ya kutengeneza mahusiano mazuri na Timu hiyo ya Uingereza pia kujiweka katika mazingira ya wachezaji wake kuonekana na Klabu hiyo plus mawakala wa wachezaji kutoka nje.Mashindano haya yapo kila pembe ya dunia ila wenzetu kwa kuwa huangalia kwa jicho angavu la maono ya mbali wakakubaliana yawe yanafanyika katika kipindi cha Pre-season.
Yapo makombe mbali mbali ya wadhamini hufanyika kipindi hicho kama Audi Cup na Emirates Cup. Kuna sababu mbalimbali ambazo hazihitaji nguvu kuzijua maana afadhali kuchakaza nguo kuliko akili;
Moja, kuvipa vilabu nafasi ya kujiandaa ili kuwa na mechi zenye ushindani kukabiliana na msimu mpya wa ligi.
Mbili, kuwapa makocha nafasi ya kuangalia mapungufu na utimilifu wa vikosi vyao wanapokutana na timu mbalimbali katika kipindi hicho ili kutoa mwanya wa kufanya maboresho kama yanahitajika.
Tatu, kuwapa wachezaji nafasi ya kurudisha fitness zao maana wengi huwa wametoka likizo walizopewa na Vilabu vyao.
Nne, mashabiki kutokuwa na presha za roho kwa kuomba dua kila saa wachezaji wasiumie kipindi kile ligi zao zikiwa zinaendelea ilihali tuwaone wakitumika katika mashindano ambayo tunahitaji mafanikio zaidi.
Haijalishi meno yanaung’ata ulimi mara ngapi lakini bado vinaishi mdomoni pamoja, TFF bado hawajachelewa kukaa na waandaji wa mashindano haya kuangalia tena jinsi gani na namna bora ya kuboresha ufanyikaji wa shindano hili ili lisiwe linafanyika kipindi hiki ambacho kila timu inayoshiriki ligi kuu inaangalia mipango iliyojiwekea katika ligi. TFF mjuwe wazi kabisa kama binadamu kaamua tu kukuongelea vibaya hata kwa misimamo mizuri unayoitoa usishangae hata ukijua kuogelea utaambiwa unawatimulia vumbi wakati unaogelea.
Ni jukumu kuu la TFF kulinda maslahi ya hivi vilabu na kuangalia uelekeo wao kama nilivyotanabaisha huko juu na kukaa navyo kushauriana, sijasema haifanyiki hivi ila NASHAURI tu kwa utimilifu wake haya pia yaendelee kutendeka.
Tunajua ubinadamu kazi japo hakuna mshahara juu ya hilo TFF wasichukulie ule msemo wa tuna kikosi kipana kuona ni sawa kwa hivi vilabu kushiriki mashindano zaidi ya haya yaliyopo katika kalenda yao kwa kuruhusu haya mashindano yenye altenatives/options za muda wa kufanyika na kukubali vishiriki katika majira haya ambayo ligi kuu inatimua vumbi nchini kwetu Tanzania na kwinginepo. Waungwana naomba mlichukuwe hili, Inafahamika vizuri kabisa mtu anayependa ukweli sio tu atawapenda wabaya wake wakimwambia ukweli pia atawachukia rafiki zake wasipomwambia ukweli.