Kuna mengi ya kujifunza kwenye safari ya Arsene Wenger akiwa Arsenal. Watu wengi hatukumjua kitu ambacho kilifanya tusimwamini kabisa.
David Dein pekee alikuwa na imani dhidi ya Arsene Wenger, ungeanzaje kumwaminisha shabiki kuwa kocha anayetoka katika ligi ƴya Japan angekuja kuipa mafanikio Arsenal?
Hakuna mafanikio yaliyoonekana mbele ya mashabiki wa Arsenal, lakini hii ilikuwa tofauti kwa mkurugenzi mtendaji mkuu wa klabu David Dein.
Aliamini Arsene Wenger anauwezo wa kuwa mfalme wa Arsenal, Arsene Wenger anauwezo wa kuwa nembo kubwa ya klabu ya Arsenal na angeangwa kwa heshima.
Kinachotokea leo ndicho kitu ambacho David Dein alikiona miaka 22 iliyopita. Leo hii kila mmoja anamtambua Arsene Wenger kama nembo kubwa ya Arsenal kutokana na mafanikio makubwa aliyowapa Arsenal.
Leo hii anaagwa kwa upendo ndani ya kikosi cha Arsenal. Hakuna aliye na chuki naye tena anaondoka kwa heshima huku akiwa anatabasamu huku mashabiki wakiumia.
Uungwana umewajaa ndani yao , uungwana ambayo huku kwetu tumeshindwa kuuishi kabisa.
Unaikumbuka Azam Fc iliyopanda daraja mwaka 2005? Hapana shaka jina la John Bocco ndilo litakuwa la kwanza ukiikumbuka Azam FC hiyo.
Azam FC ambayo ilikuwa inapigana kila siku ili kupanda daraja, miguu ya kina Bocco ilisurubishwa kiwanjani. Jasho likatiririka kwa wingi na pumzi ilikuwa kubwa katika vifua vyao mpaka timu ikapanda ligi kuu Tanzania bara.
Hakuwahi kuiacha au kufikiria kuisaliti timu yake, aliendelea kuwa mtumishi mwenye adabu mbele ya mfalme Azam FC.
Alifanya kila lililokuwa ndani ya uwezo wake kuhakikisha Azam FC inafanya vizuri ndani ya ligi kuu Tanzania.
Timu ikafanikiwa kuingia katikati ya mafahari wawili wa soka nchini ( Simba na Yanga). Tukaibeza na wengine tukaiona Azam FC ndiyo itakuwa mshindani sahihi wa hizi mbili ambazo kila mwaka hubadilishana ubingwa.
Azam FC ilifanikiwa kuchukua ubingwa mbele ya Simba na Yanga, ikawa mwiba mchungu kwa timu hizi mbili.
Mechi ya Azam FC dhidi ya hizi timu mbili ikawa mechi kubwa na yenye ushindani mkubwa, na kila jicho lilimtazama John Bocco kama muuaji wa hizi timu mbili kubwa.
Alijua vizuri sana namna ya kuziua timu hizi, hakuwa na huruma hata kidogo na huruma yake haikuhishia kwenye mechi hizi mbili peke yake.
Alikuwa mtu wa jicho la goli kwenye mechi nyingi alizocheza, ndiyo maana yeye ndiye mfungaji bora wa Azam FC wa muda wote.
Ndiye aliyekuwa nembo ya Azam FC, miaka kumi na mbili yuko pale, wamekuja kila aina ya wachezaji lakini waliondoka wakamuacha yeye akisimama na kuitetea Azam FC.
Walikuja kila aina ya makocha pale Azam FC lakini hakuna hata mmoja aliyesita kumpa nafasi John Bocco.
Kila kocha alitaka John Bocco awe chaguo lake la kwanza, busara na nidhamu zilimfanya awe kivutio kwa kila kocha na ndiyo maana akawa nahodha wa kudumu.
Nahodha mwenye mafanikio makubwa ndani ya kikosi cha Azam FC, mafanikio ambayo yalimpa heshima sana yeye pamoja na klabu kwa ujumla.
Heshima ambayo tulitegemea kuiona akipewa siku ambayo anaondoka pale Azam FC.
Hakupewa heshima stahiki hali ambayo ilionekana kaondoka kwa kufukuzwa pale chamazi.
Msimbazi kukawa makao mapya ambayo aliamua kuyachagua. Makao ambayo yamekuwa na faida kwake na ƙklabu kwa ujumla.
Leo hii John Bocco ni mhimili mkubwa ndani ya kikosi cha Simba magoli 14 mpaka sasa hivi ndani ya ligi kuu Tanzania bara.
Nahodha anayeongoza vyema jahazi lake kwa hekima na busara ndani yake.
Haonekani kuumia kwa kile alichofanyiwa, akili yake inatazama anachokifanya muda huu tena anakifanya kwa ufasaha.
Amegeuka kuwa kipenzi cha msimbazi na juhudi zake zikiwa kubwa atakuwa mhimili mkubwa ndani ya kikosi cha Simba siyo ajabu akawa nembo ya klabu ya Simba lakini hofu yangu hatopata heshima stahiki mpaka siku viatu vyake vitakapombana