Sambaza....

Kikosi cha timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kinaendelea kujichua jijini Dar es salaam kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika (AFCON 2019) dhidi ya Uganda utakaochezwa mwishoni mwa juma hili jijini Kampala.

Stars imeweka kambi jijini Dar es Salaam chini ya kocha mpya kutoka nchini Nigeria Emmanuel Amunike, ambaye amekua katika mazoezi kwa siku kadhaa na wachezaji wanaocheza soka la ndani.

Uganda Cranes wakiwa mazoezini

Stars inatarajia kuondoka nchini siku ya Alhamis kuelekea nchini Uganda na siku ya kesho jumatano  bechi la ufundi na baadhi ya wachezaji watazungumza na waandishi wa habari kwa ajili ya safari hiyo na kuelezea maandalizi yao.

Meneja wa Taifa Stars Danny Msangi amethibitisha kuanza kuwasili kwa baadhi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya mipaka ya Tanzania, huku shirikisho la soka nchini TFF likikamilisha taratibu za safari ya timu hiyo kuelekea Kampala, Uganda.

Taifa Stars mazoezini

“Muitikio wa wachezaji ni mzuri, na maandalizi yanakwenda vizuri, vijana wanamsikiliza mwalimu, morali ipo vizuri, tumendelea kuwapokea wachezaji kutoka nje kwa mfano Hassan Kessy ameingia jana, Samatta na Ulimwengu wameingia alfajiri,”

“Ratiba inaonesha tutaondoka Septemba 6 siku ya Alhamis saa saba mchana kuelekea nchini Uganda, na Mwalimu amesema vijana wanaendelea vizuri, tunachoomba watanzania waendelee kutuombea ili kwa pamoja tupate ushindi,” Msangi amesema.

Taifa Stars imepangwa kundi L lenye timu za Carpe Verde, Lesotho na Uganda.

Tayari imeshashuka dimbani mara mnoja dhidi ya Lesotho na kuambulia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja, huku Uganda wakiongoza msimamo wa kundi hilo, kufuatia kuifunga Carpe Verde bao moja sifuri.

Sambaza....