Baada ya kambi ya Uturuki msimu uliopita, mwaka huu Klabu ya Simba imeamua kwenda kuweka kambi kwa Madiba, Afrika ya kusini.
Klabu ya Simba imefikia katika hoteli yenye hadhi ya Nyota tano, ambayo pia ina uwanja wa mazoezi ndani yake, hotel hiyo pia ndio iliyokuwa hoteli iliyotumika na timu ya taifa ya Uingereza wakati wa kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika ya kusini.
Simba wameamua kuweka kambi kwenye hoteli hiyo yenye viwanja ndani yake vinavyojulikana kama State of the Art Sports Complex, vinavyopatikana ndani ya hotel hiyo inayomilikiwa na watu wa kabila la Bafokeng linalopatikana kaskazini mwa Afrika ya kusini.
–Muonekano wa nje wa Hoteli ya Bafokeng nchini Afrika Kusini.
Bafokeng pia wanamiliki uwanja wa Rustenburg uliotumika katika mashindano ya kombe la dunia mwaka 2010 ambao kwa sasa ndio uwanja wa nyumbani wa timu ya Platinum Stars inayoshiriki ligi kuu nchini humo.
Kiujumla Bafokeng Sports Campus hivi ni viwanja vya mazoezi vyenye hadhi ya kimataifa, ambapo timu yoyote duniani yenye hadhi ya juu inaweza tumia viwanja hivi kama sehemu ya kambi yake ya kujiandaa na msimu mpya au mashindano.
Ndani ya kambi hii unaweza pata viwanja vikubwa na vidogo, huduma za matibabu yaani hospitali na huduma ya Maladhi ya daraja la juu.
Simba sio klabu ya kwanza kuweka kambi katika viwanja hivyo, pia viwanja hivyo hutumika kuandalia mashindano ya watoto na akademi mbalimbali.
KASHFAA…
Kashfa kubwa iliyoikumba kambi na hoteli hiyo mwaka 2010 ni wafanyakazi wa hoteli hiyo kudaiwa kuiba vitu vya wachezaji zikiwemo nguo za wachezaji, medali, pesa na hata nguo za ndani.
Polisi wa Afrika ya kusini walithibitisha kuibiwa kwa pesa taslimu Paundi 500 ambayo ni sawa na zaidi ya shilingi million 1.4 za kitanzania. Polisi walifanikiwa kuwatia hatiani wafanyakazi watano na kisha kuwatupa jela miaka mitatu kwa kila mmoja na faini ya randi 6,000 sawa na paundi 524 kwa kipindi hicho.