Nyota wa Nigeria anaeongoza kwa magoli katika klabu ya Mwadui fc Raphael Aloba kabla ya Ligi haijasimama kutokana na janga la virusi vya corona amesema hakua anajua wala ana mawazo ya kuja kucheza soka nchini Tanzania lakini wakala ndie alifanya yeye kuwepo nchini mpaka leo.
Raphael Obafemi ambae Watanzania wengi wanamjua kwa jina la Obina msimu uliopita alikua visiwani Zanzibar akiitumikia klabu ya Hardrock fc ameongea na tovuti yako pendwa ya Kandanda na kufichua mpaka sasa huenda angekua mchezaji mkubwa na maarufu duniani kama walivyokua Wanigeria wenzake kama Obi Mikel na Ahmed Mussa.
Obina ” Niliondoka Nigeria nikiwa na umri mdogo huku wakala akiniambia ananipeleka Uturuki kujiunga na Academy ya Besiktas lakini hali ilikua tofauti wakala akawa mbabaishaji na nikajikuta natakatisha ndoto zangu. Nilipanga kua mchezaji nyota Nigeria na duniani kama Obi Mikel au Ahmed Mussa.
Baada ya mpango huo kufeli nikavutiwa na mpango wa kuja Tanzania ili nijiunge na Simba kama njia ya kwenda Ulaya maana nilikua najua kuna Wanigeria walipita hapa nakwenda Ulaya, nilisikia Emeh Ezechukwe alipita Simba akaenda nchini Denmark.”
Mpaka sasa Raphael Aloba Obafemi ana mabao sita na kutoa pasi tano za mabao katika michezo kumi na nne aliyoitumikia Mwadui fc huku akiwa na hamu Ligi irudi ili atimize malengo yake aliyojiwekea tangu mwanzoni wa msimu.
“Wakati Ligi inaanza nilikua na malengo ya kufunga mabao 12, mpaka sasa nina mabao 6 hivyo bado nadaiwa mabao 6. Ligi irudi tuu ili tumalizie michezo iliyobaki na malengo yangu yatimie. Lakini pia lazima nihakikishe Mwadui haishuki daraja hili ndio lengo kuu zaidi.” Raphael Obafemi.
Imani Joseph Mandu ambae ndio meneja wa Raphael Obafemi pia hakusita kuzungumzia hatma ya mchezaji wake katika kikosi cha Mwadui kutokana na mkataba wa mteja wake kuelekea kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
“Mkataba wake (Raphael) unaelekea ukingoni hivyo mchezaji wangu atakua huru msimu ukiisha. Chaguo letu la kwanza ni kwa Mwadui kwanza halafu ndio tutasikiliza ofa zingine, lakini tunaipa nafasi Mwadui ya kusaini tena na kuendelea nao msimu ujao.
Mteja wangu ana ofa mbili mezaji mezani mpaka sasa, na timu zote zipo Ligi Kuu mpaka sasa hivyo lolote linaweza kutokea dirisha la usajili litakapofunguliwa.” Imani Mandu alimalizia ambae pia anawasimamia wachezaji wengine kama Beka Bakary na Ally Ramadhani.