Wakati Timu ya Kandanda ya Tanzania ( Taifa Stars) ikitaraji kucheza mchezo wake wa tatu katika kundi la Saba kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika-CAN 2019 nchini Cameroon siku ya Ijumaa hii, vinara wa kundi hilo Uganda watakuwa nyumbani kuwakabili Lesotho katika mchezo mwingine mwingine muhimu kwa kila timu.
Kumbuka, kila timu imecheza michezo miwili tu katika kampeni hiyo ya kwenda Cameroon mwakani, na timu moja tu iliyopoteza mchezo ( Visiwa vya Cape Verde), timu moja tu iliyopata ushindi ( Uganda) na timu tatu hazuijaoteza mchezo ( Tanzania, Lesotho na Uganda)
Uganda wanaongoza kwa faida ya ushindi muhimu ugenini dhidi ya Cape Verde, Juni mwaka jana waliposhinda 1-0, na wapinzani hao wa Ijumaa wa Stars wanaweza kuutazama mchezo huu kama dira ya kufahamu kama wanaweza kufuzu au laa! Licha ya kuwa timu pekee iliyopoteza mchezo katika kundi-tena nyumbani, nchi hiyo ndogo ya Magharibi mwa Afrika bado itaendelea kuwa tishio kwa Stars.
Cape Verde ililazimisha sare ya kufungana 1-1 na Lesotho ugenini mwezi uliopita na hivyo ilifanikiwa kupata alama yake ya kwanza katika kundi na huku wakifahamu Uganda yenye pointi nne ikiikabili Lesotho yenye alama mbili-ushindi wao dhidi ya Stars unaweza kuwafanya kukamata nafasi ya pili.
Ni hivyo pia kwa Stars, ikiwa na michezo miwili nyumbani dhidi ya Cape Verde wiki ijayo na Uganda katika game ya mwisho ya kundi, Stars inapaswa kupigana kufa na kupona ili kuhakikisha walau wanapata alama nne katika michezo miwili dhidi ya Cape Verde.
Sare ugenini yatakuwa matokeo, na ushindi nyumbani wiki ijayo yatakuwa matokeo yanayoweza kuwasukuma nje ya kinyang’anyiro Cape Verde na huku Uganda na Lesotho wakitaraji kucheza mara mbili ndani ya siku tano upo uwezekano mkubwa wa kuongoza kundi kufikia Jumatano ijayo.
Kocha, Emmanuel Amunike ni mshindi kiuchezaji wa Mataifa ya Afrika hivyo atakuwa na uzoefu mkubwa wakati atakapoingoza Stars dhidi ya Cape Verde na katika ili lazima akubali kuitoa ‘sadaka’ mechi moja kati ya mbili zijazo. Cape Verde ni timu iliyokuwa vizuri kimpira na ninaamini itakuwa moja ya mechi ngumu sana kwa Stars na huenda wakapoteza kama hakutakuwa na umakini-kabla na wakati wa mchezo ukiendelea.
Kwa mtazamo wa kimpira na matokeo, Stars inatakiwa kwenda Cape Verde kwa lengo moja tu-kutopoteza mchezo kwa namna yoyote na alama moja ni kubwa mno hivyo wanapaswa kutumia mbinu ya kujilinda na kushambulia kwa tahadhari katika ulinzi ili wenyeji wao wasifanikiwe kupata ushindi ambao utawafanya kuwa juu ya Stars kwa alama mbili zaidi.
Hii si fainali, lakini natazama mchezo huu kama hatma ya kundi, na kupoteza kwa Stars litakuwa pigo kama yale mengine yaliyoendelea kuwakuta katika kipindi cha miaka 38 iliyopita. Stars inapaswa kufahamu sasa ni aina gani ya matokeo yanayoweza kuwasaidia.
Ndiyo, ushindi ni target ya kwanza kwa makocha wengi lakini katika michezo kama hii sare ugenini ni bora kuliko hivyo Stars inapaswa kucheza kwa kujilinda ugenini na kuja kufunguka nyumbani. Pointi nne dhidi ya Cape Verde ni matokeo mazuri mno, lakini yanahitaji mikakati ya kuyatafuta. Isiende kushambulia, ikajilinde dhidi ya Cape Verde na kucheza kwa tahadhari kubwa.