Leo Yanga wamefanikiwa kuifunga Azam Fc ambayo ilikuwa haijapoteza mechi yoyote msimu huu.
Yanga leo kwenye karatasi ilionekana itacheza mfumo wa 4-3-3 lakini uwanjani ilikuwa tofauti kwa sababu walikuwa wanacheza 4-5-1 na 4-2-3-1. Wakati Azam Fc walianza na mfumo wa 4-4-2 baadaye wakaja kucheza 4-1-4-1 na mwishoni wakarudi kwenye mfumo wa 4-4-2.
Wakati dakika kumi za kwanza zinaanza Yanga walikuwa wanacheza 4-5-1 ambapo walikuwa wamekaa nyuma kwa kiasi kikubwa na Azam Fc walikuwa wanacheza mfumo wa 4-4-2.
Yanga walijaza viungo wengi katikati, Said Makapu , Papy Kabamba na Raphael Daud ambapo alikuwa anakuja katikati wakati timu inashambuliwa na kuifanya timu ya Yanga iwe na viungo watatu katikati ya uwanja dhidi ya viungo wawili wa Azam Fc ambao walikuwa ni Stepahano Kingue na Salum Abubakar “sureboy”.
Hivo katikati kukawa hakuna uwiano, ikawa 3 v 2 ( yani viungo watatu wa Yanga dhidi ya viungo wawili wa Azam Fc)
Ugumu ukaonekana kwa Azam Fc wanaposhambulia kupitia katikati hivo wakawa wanatumia upande wa pembeni kushoto kwa Bruce Kangwa ambapo ndipo walifanikiwa kupata goli la kwanza.
Baada ya goli la kwanza Yanga waliubadili mfumo wao wa 4-5-1 na kuuweka katika umbo la 4-2-3-1. Ambapo mabeki walibaki kuwa Yondan na Vincent waliocheza kama mabeki wa kati, mabeki wa pembeni wakabaki kuwa Hassan Kessy kulia na Gadiel Michel kushoto.
Ila kiungo wa kuzuia akabaki kuwa Said Makapu ambapo Papy Kabamba alicheza kama box to box ambapo alikuwa na uwezo wa kupanda na kushuka nyuma kusaidia kukaba. Raphael Daud akawa anatokea pembeni kulia wakati timu inashambulia na wakati timu inashambuliwa alikuwa anarudi katikati kuongeza idadi ya viungo wa kati.
Ibrahim Ajib alikuwa anashuka katikati kuchukua mipira na kumwacha Chirwa akicheza kama mshambuliaji peke yake mbele wakati Emmanuel Martin akitokea pembeni kushoto.
Kitendo cha Ibrahim Ajib kushuka katikati kuchukua mpira kulikuwa na faida kwa Yanga,kwa sababu alikuwa anashuka bila mtu aliyekuwa anamkaba “kumu mark”. Kazi hii alitakiwa aifanye Stephano Kingue lakini alimwacha huru kitu kilichosababisha atengeneze goli la kwanza.
Goli ambalo kwanza makosa yalianza kwa mabeki wa Azam Fc kutokuwa na umakini wa kuzuia ile pasi na kukosa mawasiliano kati ya mabeki na kipa.
Kipa alifanya kosa kutoka kufuata mpira bila kuwa na uhakika wa kuuchukua. Kanuni ya kwanza ya ƙkipa anapotokea mpira awe na uhakika wa kuucheza ule mpira lakini Chirwa alimlazimisha Razack Abarola kufanya makosa.
Baada ya goli la kusawazisha , Yanga walibaki kwenye mfumo ule ule wa 4-2-3-1 na Azam Fc wakaendelea kubaki kwenye mfumo wao wa 4-4-2.
Hali ambayo iliwafanya Yanga wazidi kuwatala Azam Fc katika eneo la kiungo wa kati ambapo uwiano uliendelea kutokuwa sawa kwa kuwa na idadi ya viungo 3 dhidi ya 2 wa Azam FC. Safari hii Raphael Daud akiwa anacheza eneo la katikati kulia mwa uwanja. Na goli la pili lilianzia katikati mwa uwanja ambapo Papy Kabamba alitoa pasi kwa Gadiel Michel na akafanikiwa kufunga.
Baada ya Mwalimu wa Azam Fc kuona amezidiwa aliamua kumtoa mshambuliaji na kumwingiza kiungo.
Baada ya Hoza kuingia Azam Fc walibadirika kutoka kutumia mfumo wa 4-4-2 mpaka kutumia mfumo wa 4-1-4-1 ambapo mabeki wa nyuma walibaki kuwa Yakubu na Agrey waliocheza kama mabeki wa katikati , beki wa kulia akacheza Himid na beki wa kushoto akacheza Bruce Kangwa.
Kiungo wa nyuma alikuwa stephano kingue na viungo wawili waliocheza mbele ya Stephano walikuwa Salum Abubakar na Hoza, pembeni kulia akawa anacheza Atta-Agyei na pembeni kushoto akawa anacheza mahundi, mbele akabaki akicheza Shaban Chilunda.
Yanga wakarudi kwenye umbo la 4-5-1 ambapo walicheza hivo hivo kipindi cha pili chote.
Kipindi cha pili Azam FC walirudi katikati umbo la 4-4-2 baada ya Kingue kutolewa na kuingizwa Mbaraka Yusuph ambapo mbele alicheza na Chilunda. Hata baada ya Chilunda kutoka na kuingia Paul Peter walibaki kuwa na mfumo huo huo wa 4-4-2 na yanga wakabaki na 4-5-1 ambapo walijilinda kwa utulivu mpaka mwisho wa michezo.
Hitimisho: Yanga waliingia kama underdogs kwenye mchezo huu hali ambayo waliipokea na kucheza bila presha hivo kuwa na utulivu kwenye maamuzi yao, wakati Azam Fc walijiamini sana mpaka wakawa na makosa mengi hasa hasa kwenye safu ya ulinzi.