Uongozi wa klabu ya soka ya Singida United umetangaza benchi jipya la ufundi ambalo litaongozwa na Makocha wawili kutoka Serbia kwa ajili ya kuifundisha timu hiyo, makocha hao ni Popadic Dragan ambaye ni Kocha Mkuu ameamua kuja na mwenzake ambaye atakuwa Msaidizi, Dusan Momcilovic.
Usajili wa makocha hawa umefanikiwa ikiwa ni baada ya klabu hiyo kutokuwa na Kocha Mkuu tangu kuondoka kwa Hans Van Der Plujim ambaye alitimkia Azam FC ya jijini Dar es Salaam na timu kubaki kwa Hemed Moroko na Shadrack Nsajigwa.
Mkurugenzi wa Singida United Festo Richard Sanga, amesema kuwaleta makocha hao ni moja ya mikakati yao kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano ya Ligi kuu na michuano ya SportPesa Super Cup inayotazamiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
“Nadhani ukimuondoa Hans huyu ndiye kocha ambaye ana CV kubwa zaidi hapa nchini, wengi mtamkumbuka alipokuwa Simba, amekuja kwa ajili ya kutusaidia kufanya vizuri kwenye ligi na michuano ya SportPesa ambayo mwaka huu tunataka kuwa mabingwa, sasa benchi la ufundi litaongozwa na hawa makocha nah ii ni mikakati katika kuifanya Singida United kuwa bora,” amesema.
Kwa upande wake kocha Popadic amesema walipigiwa simu na Rais wa Klabu Mwigulu Nchemba akiwataka kuja kuisaidia timu na wao wakakubali, amesema hii sio mara ya kwanza kuja Afrika na imani yake ni kufanya vizuri katika michezo iliyopo mbele yao.
Popadic ni nani?
Popadic aliiwezesha Simba kutwaa mataji saba kati ya mwaka 1994 na 1996, mawili ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame miaka 1995 na 1996, ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo, 1994 na 1995, ubingwa wa Ligi ya Muungano mwaka 1994 na ubingwa wa Kombe la Nyerere miaka ya 1994 na 1995.
Popadic aliingia Simba akichukua nafasi ya kocha mzawa,
Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ aliyekuwa akisaidiwa na Mhabeshi,
Entenneh Eshenteh ambao kwa pamoja waliifikisha timu hiyo Fainali ya Kombe la
CAF mwaka 1993.