Klabu ya soka ya Singida United ya mkoani Singida imeweka wazi mipango yake katika dirisha dogo la usajili, ambapo imepanga kusajili wachezaji sita pekee huku wanne kati ya hao wakitokea nje ya Tanzania.
Mkurugenzi wa Singida United Festo Richard Sanga amesema usajili huo upo katika Programu ya klabu hiyo ‘Make Singida United Great Again’ ambayo inalenga kukiongezea kikosi chao nguvu na kuwa na uwezo sawa au zaidi ya ule waliokuwa nao msimu uliopita.
“Tuna project ambayo tunaitengeneza, lazima tuifanye Singida United iwe nzito kwa uzito ule ule au zaidi ya tuliokuwa nao mwaka jana, kwa hiyo dirisha dogo tunategemea kuongeza wachezaji sita, wawili wa ndani na wanne kutoka nje ya nchi, mmoja anatokea Norway ni mzaliwa wa Liberia na mwingine anatokea Ghana anaitwa Mensah,” Sanga amesema.
Aidha Sanga amewaomba mashabiki na wapenzi wa klabu ya Singida United kuhakikisha wanaiunga mkono timu yao hata pale wanapokuwa hawana matokeo mazuri kwani wao ni sehemu ya klabu.
“Kwa mashabiki watambue kuwa mpira una matokeo ya aina tatu, ni kosa kwenye kanuni za kandanda kutembea na matokeo mfukoni, watambue kwamba timu hii kuna siku iliwafurahisha na ipo siku itawahuzunisha ndo mpira ulivyo, uvumilivu ni muhimu na ni lazima waiunge mkono timu,” amesema.
Sanga ameongeza kuwa kwa sasa wapo katika mkakati mzito wa kutafuta wadhamini wapya na pengine kuanzia Januari mwakani wataingia mikataba na makampuni makubwa ambayo yameridhia kuidhamini.
Amekanusha taarifa za klabu hiyo kufilisika kwa kusema kuwa bado wanapambana kutafuta fedha zaidi ili waweze kuwa bora kadri siku zinavyosonga mbele.