Sambaza....

BAADA ya kukusanya pointi 45 katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza na kuongoza ligi kwa tofauti ya alama zaidi ya kumi dhidi ya Tanzania Prisons na Yanga SC, timu ‘iliyokufa‘- Moro United FC ilishindwa kupata walau alama 15 katika michezo 15 ya mzunguko wa pili ili watwae ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara mwaka 2005.

Kushindwa kwao si tu kulitushangaza wengi tuliokuwa tukienda Jamhuri Stadium, Morogoro kuipa sapoti, bali kulimchefua mno aliyekuwa mmiliki wa klabu hiyo- mfanyabiashara na tajiri wa mafuta, Merey Balhabou ambaye aliamua kuachana nayo na si tu hivyo alijiondoa kabisa katika mambo ya soka.

HUJUMA…

Ukimtoa, Salum Sued ‘Kussi‘ wachezaji wengine watano waliokuwa wakiunda ‘ngome ngumu‘ ya ulinzi walihusika kujiondoa kwa Balhabou katika medani ya soka. Golini alikuwepo Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Jumanne Ramadhani, Lulanga Mapunda, Kussi na Waziri Mahadhi ‘Mendieta‘ aliyekuwa akitumika kama kiungo-mlinzi.

Safu hii ya ulinzi ‘iliiangamiza‘ Moro na kocha Mkenya, James Siang‘a alipokuja kustuka muda ulikuwa umekwisha. Kilichokuwa kikifanyika ni- wachezaji hao kwa kushilikiana na baadhi ya viongozi wa timu hiyo- waliahidiwa kusajiliwa na klabu moja kubwa nchini kama wataisaidia kutwaa ubingwa.

Moro United ile iliyofahamika pia kama ‘Chelsea ya Bongo‘ kutokana na usajili bora na wa gharama, huku wachezaji wakilipwa mishahara mizuri na posho za juu ilihujumiwa kwa namna ya kuvunja moyo wa mmiliki wao.

Walinzi walihusika na mchezo huo mchafu katika soka: ilikuwa wanaruhusu goli la kizembe na timu yao ikiwa nyuma mchezoni wanacheza vizuri zaidi ya mchezo uliopita. Timu ambayo ilishinda michezo yote ya mzunguko wa kwanza ilicheza michezo kumi na kushinda mara moja tu katika mzunguko wa pili, na michezo isiyozidi mitatu kati ya 15.

Mwisho wa msimu Yanga ilitwaa ubingwa ikiwa na pointi 57 au 59 kama sijapoteza kumbukumbu. Ivo, Nsajigwa, Lulanga na Mendieta wakajiunga na timu hiyo ya Dar es Salaam na kuthibitisha yale yalikuwa yakisemwa- wahujumu. Wanaweza kuendelea kukataa lakini ukweli hautobadilika kamwe.

AZAM FC…

Mwaka mmoja uliopita kulikuwa na tetesi ya mmiliki wa Azam FC kutaka kuiacha timu hiyo. Sababu kubwa ni klabu kuendelea kudumaa licha ya uwekezaji mkubwa unaofanyika. Alikuwa sahihi kwasababu watu waliokuwa wamepewa nafasi za uongozi klabuni hapa walitazama zaidi maendeleo yao binafsi kuliko ukuaji wa klabu.

Mfano, Saad Kawemba chini ya utawala wake Azam FC ilipoteza kiasi kikubwa mno cha pesa kutokana na usajili wa hovyo wa makocha na wachezaji kutoka ng‘ambo.

Wachezaji wa kigeni walikuwa wakisajiliwa kwa gharama kubwa na kulipwa mishahara ya juu pasipo kujali viwango vyao. Na kuna wakati utawala wa Saad ulimuajiri kocha Mhispania ambaye alikuwa na wasaidizi wasiopungua wanne nao pia walitokea Hispania. Lakini wengi waliondolewa wakati mikataba yao ikiwa mirefu na kuitia klabu hasara.

SINGIDA UNITED…

Achana na golikipa Manyika Peter Jr ambaye ameamua kujiondoa katika timu hii kwasababu za kutolipwa mishahara yake kwa zaidi ya miezi minne, ndani ya timu hii zaidi ya robo tatu ya wachezaji wanadai si tu mishahara, posho bali hadi pesa zao za usajili.

Festo Sanga ambaye ni mkurugenzi wa klabu amegoma kuwaajiri wafanyakazi wengine muhimu katika klabu na hivyo 90% amekuwa akisimamia yeye. Umeneja wa timu yeye, usemaji wa timu yeye, ukatibu yeye, yaani kila kazi amekuwa boss ni yeye.

Bwana Sanga akitambulisha udhamini

Unaweza kujiuliza Kwanini Singida United licha ya kuongoza kwa udhamini katika soka la Tanzania lakini ndani ya uwanja imekwama? Wachezaji wana njaa mno, ndiyo ukweli huo. Wachezaji wanakopwa na hawalipwi wanapojiunga na timu hiyo. Kwanini wakati klabu ina wadhamini zaidi ya saba?.

Mawazo na malengo ya mmiliki ni kuifanya Singida United kumiliki uwanja wake wa kisasa na kujiendesha bila shaka, amewavutia wadhamini na wameiunga mkono kwa kiasi kikubwa mno lakini mtu mmoja- Sanga amekuwa kikwazo na kama mmiliki ataendelea kufumba macho na kuziba masikio aelewe klabu yake ipo karibu na mlango wa kuzimu- itarudi ilipokuwa kwa miaka 15 iliyopita.

Moro United ilihujumiwa na viongozi ambao Merey aliwaamini pamoja na baadhi ya wachezaji, Azam FC ilidumazwa mno na utawala wa Kawemba, na kwa jinsi mambo yanavyokwenda, Sanga ni mtu anayekaribia kuiua Singida United.

Kama wachezaji 15 hadi 20 wanadai klabuni jambo hilo ni hatari kwa ukuaji wa klabu. Pesa za wadhamini zinakwenda wapi ikiwa wachezaji zaidi ya robo tatu wanadai katika timu- pesa za usajili, mishahara, posho na bonasi?

Sambaza....