Baada ya droo ya michuano ya kombe la FA maarufu kama Azamsports Federation Cup kufanyika na sasa Shirikisho la soka nchini TFF wametoa ratiba rasmi kwa vigogo waliotinga robo fainali.
Tayari ratiba ya michuano hiyo imeshatoka na sasa michezo ya robo fainali itapigwa kati ya Aprili mbili mpaka Aprili nane mwaka huu. Washindi wa hatua hii watakwenda nusu fainali na michezo hiyo itapiga katika viwanja vya Nang’wanda Sijaona Mtwara na Liti mkoani Singida.
Aprili mbili mwaka huu Singida Big Stars watakua wenyeji wa Mbeya City katika uwanja wa Liti na kufungua pazia ya michezo ya robo fainali. Azam Fc wao watashuka dimbani Chamanzi siku inayofuata kwa kuwakaribisha Kagera Sugar katika uwanja wao wa Azam Complex.
Simba wao watakua uwanja wake wa nyumbani Uhuru kuwakaribisha “Mbogo maji” Ihefu katika mchezo utakaopigwa April saba. Msimu uliomalizika Simba walitolewa nusu fainali na Yanga katika michuano hiyo.
Mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga wao ndio watatamatisha michezo ya robo fainali kwa kuwakaribisha Geita Gold Chamanzi katika dimba la Azam Complex.
Bingwa wa kombe hilo ndio atakwenda kuwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ni wazi Azam Fc na Singida Big Stars watawekeza nguvu zao katika kombe hili ili kuweza kupata uwakilishi wa Kombe la Shirikisho Afrika.