Sambaza....

Klabu ya Singida Big Stars imeuzwa na kununuliwa na Fountaine Gate ya Dodoma na hivyo kubadilishwa jina na kuitwa Singida Fountaine Gate Fc.

Wakiongea mbele ya waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam viongozi wa timu zote mbili wamethibitisha hilo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Akademi ya Fountain Gate, Japhet Makau ambaye kwa sasa ni Rais wa klabu hiyo kwenye muundo mpya, alisema; “Tumeona fursa ambayo imetokea Singida BS, baada ya kuona watafute mtu wa kuichukua,'”

“Singida BS, kwetu tumeona ni sehemu nzuri na kuona kuichukua Singida BS, timu kubaki Singida kwetu hiyo sio changamoto kabisa na Fountain inaweza kuwa Tanzania nzima,” alisema.

Kikosi cha Singida Big Stars kwa pamoja kwa msimu 2022-2023.

Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Singida BS, John Peter alisema katika mkutano huo “Siku hizi gharama za uendeshaji wa klabu ni kubwa sana, tumetafakari hili pamoja na changamoto tulizonazo, tukatafuta na kuona nani wa kumtua mzigo, tukaona tuungane na hawa ndugu zetu wa Fountain, tulizungumza nao hawa wenzetu ambao wanajua kuhusu mpira kwa sababu wamekuwa na timu ya daraja la kwanza na hata Ligi Kuu kwa upande wa Wanawake,”

“Tumewasogelea ili kufanya nao biashara ili kuendeleza furaha ya mpira, tumekaa nao mezani na kukubaliana vipengele vya kuchukua timu na kununua, moja na sharti kubwa ni timu kubaki Singida na lazima neno Singida libakie kwenye timu ili kuenzi,” alimalizia.

Baada ya Singida Big Stars kumaliza nafasi ya nne na kujihakikishi nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika mwaka huu imewalazimu kuungana na Fountaine Gate ili kukidhi matwaka ya CAF wakizitaka timu shiriki kuwa na timu za wanawake.


Sambaza....