Sambaza....

Klabu ya Simba inaendelea kimyakimya kukisuka kikosi chake kuelekea msimu ujao wakianza kuangazia sehemu mbalimbali kuimarisha timu yao katika maeneo muhimu.

Wekundu wa Msimbazi wameangukia kwa shambuliaji raia wa Ghana Kwame Peprah ambae anamilikiwa na Orlando Pirates lakini kwasasa akiwa kwa mkopo katika klabu ya Martizburg.

“Simba imewasiliana na Pirates kuuliza kuhusu kupatikana kwa Kwame Peprah. Wanatafuta kumsajili kwa msimu ujao,” kilisema chanzo kikiongea na mtandao wa FAR Post.

Kwame Peprah.

“Simba ina mshambuliaji mmoja tu wa kutegemewa kwa sasa, na ni Jean Baleke Othos. Yuko kwa mkopo kutoka TP Mazembe. Ana mkopo wa mwaka mmoja. Chaguo jingine ni John Bocco, lakini anapambana na majeraha. Kwa hivyo wanahitaji mshambuliaji wa wasifu wa Kwame.” kilisema chanzo

Peprah amekosa muda wakutosha wakucheza  katika msimu wake wa pili akiwa Pirates. Baada ya kukakosa muda wa kucheza Peprah aliomba kuhamia Maritzburg United kwa mkopo wakati wa dirisha la usajili la Januari lakini huko Maritzburg pia amepata wakati mgumu kupata nafasi ya kucheza.

Mpaka sasa akiwa Martizburg amecheza mechi nane, akifunga mara moja tu.  Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alijiunga na Pirates kutoka klabu ya King Faisal FC ya Ghana kwa mkataba wa miaka mitatu. Hii ilikuwa ni baada ya  kufanya vyema katika nchini kwake Ghana kwa kufunga mabao 12 na kutoa asisti 10 katika michezo 32 katika msimu wa 2020.

Kwame Peprah katika moja ya michezo ya PSL Ligi Kuu ya nchini Afrika Kusini.

Akiwa Pirates, alifurahia zaidi kucheza chini ya makocha wake Fadlu Davids na Mandla Ncikazi. Peprah alifunga mabao tisa katika mashindano yote akiwa na Buccaneers. Mabao mawili kati ya hayo yalipatikana kwenye Kombe la Shirikisho la CAF wakati wakitinga fainali katika msimu ambao waliwato Simba Sc hata hivyo Pirates walifungwa na RS Berkane katika fainali.

Kiasi cha dola 150,000 sawa na zaidi ya miliono 300 za Kitanzania kinatajwa kuweka na Pirates ili kumuachia nyota huyo ambae msimu ujao ataingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake. Kiasi hicho pia ndio kililipwa na Pirates wakati wakimsajili kutoka King Faisal ya Ghana.

Mpaka sasa Simba imekua haina uhakika katika eneo la mbele endapo Jean Baleke atakosekana kwani Moses Phiri amekua kwenye kiwango kidogo tofauti na alipoanza msimu na hii ni baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambapo ilipelekea kukaa nje kwa muda mrefu.

Sambaza....