Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe amefichua kuwa Ligi ya Mabingwa Afrika itaanza mwezi Oktoba na kuthibitisha kutakuwa na jina jipya la michuano hiyo.
Mnamo Novemba 29, 2019, Shirikisho la Soka Afrika (Caf), lilitangaza rasmi kuanzishwa kwa Super League ya Afrika ili kuimarisha michezo barani Afrika.
Kiini cha mashindano hayo ni mapato makubwa ya kifedha, yanayotarajiwa kuzidi dola milioni 100 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu na kukuza mchezo huo barani Afrika. Mbali na kuthibitisha kuwa kwa mara yakwanza yatafanyika kabla ya mwaka kuisha, Motsepe alisema zaidi jina hilo litabadilishwa ili kuvutia wadhamini zaidi.
“Oktoba mwaka huu, Ligi ya kwanza itaanza, baadhi ya watu walikuwa wakiuliza tarehe, tunayo tayari,” alisema Motsepe wakati wa FIFPRO Africa Congress huko Gaborone, Botswana.
“Baadhi ya wafadhili wakubwa wanasema ‘historia ya Super League barani Ulaya haikuwa nzuri. Ukihusisha jina ‘super’ na mashindano ya soka, lina maana hasi.”
“Tunaweza kubadili jina, lakini kitakachofanyika Oktoba ni uzinduzi. Nitaendelea kutumia jina la ‘African Super League’. mpaka tuibadilishe,” alisema Motsepe
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza ni Simba pekee kutoka nchini Tanzania ndio watakaoshiriki. Pia kuna timu za Mamelodi Sundowns (South Africa), Al Ahly (Egypt), Petro de Luanda (Angola), TP Mazembe (DR Congo), Horoya (Guinea), Wydad Atheltic Club (Morocco), na Esperance de Tunis (Tunisia).
Tayari kikosi cha Simba kimeshaanza maandalizi ya kushiriki michuano hiyo huku wakiwa tayari wanajinasibu wameanza usajili mzito kuelelea mashindano hayo.