Baada ya kukaa misimu minne bila kuchukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara, hatimaye klabu ya Simba imefanikiwa rasmi kuwa bingwa wa Ligi kuu Tanzania bara msimu wa mwaka 2017/2018.
Hii imetokana baada ya timu ya Prisons kuifunga Yanga magoli 2-0 . Kwa matokeo hayo Simba ina alama ambazo haziwezi kufikishwa na timu yoyote kwa sasa.
Yanga imebakiza michezo mitano (5) mpaka sasa hivi ikiwa na alama 48 katika nafasi ya tatu.
Kama Yanga ikifanikiwa kushinda michezo yote hiyo mitano itakuwa imechukua alama ƙkumi na tano (15) alama ambazo ukiziongeza na alama 48 anakuwa na alama 63 ambapo itakuwa pungufu ya alama mbili za Simba ambayo ina alama 65 mpaka sasa ikiwa imecheza michezo 27.
Azam Fc inayoshika nafasi ya tatu na alama 49 haina uwezo pia ya kuzifikia alama za Simba kwa sababu wamebakiza michezo mitatu, ambapo wakishinda michezo hiyo mitatu watapata alama tisa ambazo ukiziongeza kwenye alama walizo nazo wanakuwa na alama 58.
Kwa hiyo Simba imekuwa bingwa rasmi wa ligi kuu Tanzania bara wakiwa chumbani wamelala wakisubiri mechi ya Singida United.
Mechi hii itakuwa ya kumamilisha ratiba tu na kulinda heshima kwa sababu Simba inataka kumaliza ligi ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja.
Na hiki ndicho ƙkitu pekee kinachowapeleka Singida , kuhakikisha hawapotezi mchezo huo na kumaliza ligi ikiwa haijapoteza mchezo huo.
Pia kuna baadhi ya wachezaji wa Simba wanataka kuvunja rekodi na kuweka rekodi zao mbalimbali. Mfano mzuri ni Emmanuel Okwi ambaye ana mtihani mkubwa wa kuivunja rekodi ya mtu aliyefunga magoli mengi katika msimu mmoja , ambapo inashikiriwa na mchezaji ambaye ana magoli 24 ambapo mpaka sasa Emmanuel Okwi ana magoli 20, hivi katika michezo mitatu iliyobaki Emmanuel Okwi anatakiwa kufunga magoli manne au zaidi ili kuifikia na kuivunja rekodi hii.