Sambaza....

Wekundu wa Msimbazi Simba wamevuka na kwenda katika hatua ya nusu fainali ya kombe la FA kwa kishindo kikubwa baada ya kuibugiza mabao mengi Ihefu Fc na sasa watakutana na Azam Fc.

Simba imefanikiwa kuifunga Ihefu Fc mabao matano kwa moja katika Dimba la Azam Complex na kufuzu kwenda nusu fainali na sasa watakutana na Azam Fc  ambao wao walishafuzu baada ya kumfunga Mtibwa Sugar mabao mawili kwa sifuri.

 

Alikua ni mshambuliaji Jean Baleke aliyepeleka kilio kwa Mbogo Maji baada ya kufunga mabao matatu “hatrick” akisaidiwa na Said Ntibazonkinza na Pape Sakho waliofunga bao moja kila mmoja na kukamilisha mabao matano.

Baleke alifunga mabao hayo katika dakika ya 2, 15 na 28 za mchezo huo wakati Saidoo alifunga dakika ya 39 na Sakho akifunga katika dakika ya 94. Bao pekee la Ihefu lilifungwa na Raphael Daud Loth katika dakika ya 60 akiunganisha krosi safi kutokana na mpira wa faulo uliopigwa na “Dead Ball Master” Never Tigere.

Vita ya Simba na Ihefu ni kama bado haijakwisha kwani siku tatu mbele yaani tarehe kumi watakutana tena mkoani Mbeya Mbarali katika mchezo wa Ligi Kuu ambapo Ihefu sasa ndio watakua wenyeji wa Mnyama Simba.

Sambaza....