Sambaza....

Msemaji wa klabu ya Simba Ahmed Ally amesema anawashangaa wale wanaisema Simba kwamba haikucheza vizuri katika mchezo dhidi ya Vipers ugenini.

Simba ilipata alama tatu ugenini katika mchezo wake wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers licha ya kutokucheza vyema kama ambavyo Simba imezoeleka lakini msemaji huyo wa Simba amesema kuna kuchagua kucheza vizuri au kupata alama tatu.

 

Ahmed Ally “Ukiutazama mchezo dhidi ya vipers sijui wanaosema tumecheza vibaya wanatumia vigezo gani.

Kwa takwimu za mchezo ule sisi tulicheza na kumiliki mpira kwa asilimia hamsini na wao pia asilimia hamsini. Lakini pia katika mchezi ule malengo yetu yalikua ni alama tatu. Mechi dhidi ya Horoya tulicheza vyema lakini hatukupata matokeo sasa utachagua ucheze vizuri au upate alama tatu.”

Lakini pia Ahmed amewatoa hofu mashabiki wa Simba kuelekea mchezo ujao kwa kuahidi soka safi na alama tatu kwani watakua nyumbani sehemu ambayo wameizoea.

“Hata mchezo dhidi ya Raja Casablanca licha ya kula bao tatu lakini bado tulicheza vizuri. Hivyo mchezo ujao dhidi ya Vipers ndio tutajua tucheze vipi. Maana tutakua eneo letu la kujidai na tutacheza kandanda safi na alama tatu tutabeba,” Ahmed Ally.

Simba inatarajiwa kuikaribisha Vipers siku ya Jumanne Machi saba katika uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sambaza....