Kuelekea mchezo mgumu wa robo fainali ambao Wekundu wa Msimbazi Simba watakua nyumbani kuwakaribisha mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika Wydad Casablanca mwenyekiti wa Klabu hiyo ametema cheche.
Murtaza Mangungu mwenyekiti wa Klabu ya Simba amesema wao walishajiandaa muda mrefu na mipango yao inakwenda sawa kabisa kuelekea mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa huku akijivunia ushirikiano wa Wanasimba wote na hivyo watanarajia matokeo mazuri.
“Mipango yetu inakwenda sawa kabisa kuelekea katika mchezo huo, hatujaanza maandalizi leo kawaida yetu tunaanza maandalizi tangu baada ya msimu kuanza na baada ya kuvuka makundi tulijua tunaelekea robo fainali,” alisema na kuongeza
“Tunashiriliana na watu wote katika kila ngazi kwenye klabu na hivyo tunategemea tutapata matokeo chanya katika mchezo huo kutokana na jins ambavyo tunafanya mambo yetu,” Murtaza Mangungu Mwenyekiti wa Simba.
Mwenyekiti huyo pia amesema kwa nchi hii Simba ndio ina wachezaji wenye uzoefu na michuano ya Kimataifa hivyo hana shaka wanajua nini wanatakiwa wafanye na kupata matokeo mazuri.
Murtaza Mangungu “Wachezaji wetu wapo tayari kwaajili ya mchezo na kitu kizuri wana uzoefu mkubwa na michezo hii ya Kimataifa, Simba ndio timu yenye wachezaji wenye uzoefu zaidi hapa nchini na michezo ya Ligi ya Mabingwa kwasasa. Simba imecheza robo fainali mfululizo tuambie huko kwingine kama utawapata wachezaji wa aina hiyo kwao.”
Katika hatua nyingine kiongozi huyo wa juu wa Simba ameweka sawa na kusisitiza muda wa mchezo wao ni uleule wa saa kumi jioni na hao wanaosema mchezo ni saa moja jioni wanaeneza propaganda tuu ambayo haina maana yoyote.
“Mchezo wetu utachezwa saa kumi jioni sasa huyo ambae analeta propaganda anataka tuu kuvuruga mambo, hakuna mabadiliko yoyote mchezo utachezwa saa kumi jioni kama awali ilivyoonyesha na tayari tumeshapewa ratiba na CAF,” alimalizia Mangungu
Mnyama Simba anategemea kushuka mawindoni katika uwanja wake wa kujidai wa Benjamin Mkapa majira saa kumi jioni April 22 Jumamosi hii kuvaana na Wydad Casablanca kutoka Morocco. Simba wanapaswa kuwa makini kwani wanacheza na bingwa mtetezi lakini pia ndugu zao Raja Casablanca walitua kwa Mkapa na Mnyama akapokea kipigo cha bao tatu kwa sifuri.