Mabingwa wa soka Tanzania bara, Simba SC, wanataraji kushuka dimbani leo kuwavaa Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa fainali ya michuano ya Sportpesa Super Cup utakaopigwa majira ya saa 9:00 alasiri kunako uwanja wa Afrah mjini Nakuru
Simba SC, imefika fainali baada ya kuzitoa timu za Kakamega homeboys na Kariobang Sharks za Kenya kwa njia ya penati kufuatia sale ya 0-0 ndani ya dakika 90, za kawaida
Kwa upande wa Gor Mahia maarufu kama K’Ogaro wao walifaika hatua hiyo baada ya kuzifunga timu za JKU ya Zanzibar kwa mabao 3-0 kisha kuifunga Singida United mabao 2-0
Katika mchezo wa leo Simba SC, itaongozwa na Kocha msaidizi, Masoud Djouma Irambona, baada ya aliyekuwa Kocha mkuu Mfaransa Pierre Lechantre kutimka kunako kikosi hicho
Lechantre na msaidizi wake Aymem Mohammed raia wa Tunisia, waliishuhudia Simba ikitinga fainali wakiwa jukwaani ilipomenyana na Kakamega homeboys katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Alhamisi ya wiki hii kabla ya Ijumaa kurejea kwao baada ya kutoelewana na uongozi wa klabu hiyo
Bingwa wa Sportpesa atapata kitita cha dola za Marekani 30,000 sanjari na nafasi ya kwenda kucheza mchezo wa kirafiki na klabu ya Everton kunako dimba la Goodson Park jijini Liverpool, Uingereza
Mshindi wa pili atazawadiwa dola 10,000, mshindi wa tatu dola 7,500 mshindi wa nne dola 5,000 huku timu zingine zikipata kifuta jasho cha dola 2,500
Gor Mahia ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo, ambapo mwaka jana waliwafunga AFC Leopards kwa mabao 2-1 katika fainali iliyopigwa kunako uwanja mkuu taifa jijini Dar es salaam, Tanzania
Kuelekea katika mchezo wa leo tayari Simba wameanika kikosi kitakashuka dimbani
(1) Aishi Manura
(2) Shimari Kapombe
(3) Yusuph Mlipili
(4) Paul Bukaba
(5) Erasto Edward Nyoni
(6) Jonas Mkude
(7) Shiza Ramadhan Kichuya
(8) Mzamir Yasin
(9) Mohammed Rashid
(10) Rashid Juma
(11) Adam Salamba
Akiba
Ally Salim
Shomari Ally
Mohammed Hussein “Tshabalala”
Mercel Bonaventure Kaheza
Moses Kitandu