Katika nchi hii upende usitake kila mtu lazima ni Yanga au Simba, hata kama yupo upande wa timu yoyote ambayo si kati ya hizi basi mtu huyo lazima anavichembechembe vya ushabiki wa mojawapo wa miamba hii ambayo inaonekana ni mikubwa zaidi. Hata imefikia hatua katika uendeshwaji wa vyama vya mpira wa miguu kuwa na watu wenye itikadi za timu hizi pia ndani yake, yawekezana hadi kwa waamuzi pia. Maofisini, Mashuleni hadi Bungeni, Mbunge anaweza kuwa CCM au Chadema au CUF lakini wanakutana kwenye Simba SC au Yanga SC. Ushindani wake umepachikwa jina la “Watani wa Jadi”.
– Mashabiki wa Simba wakiwakebehi Yanga
Hivi karibuni umezuka mjadala mkubwa baada ya Yanga kufanya tukio waliloliita Kubwa Kuliko, ambayo ilikuwa na lengo la kuchangisha fedha kwaajili ya uendeshaji wa timu hiyo. Malengo yalikuwa kutafuta Bilioni 1. Katika moja ya wachangiaji alikuwa ni Bilionea Rostam Aziz ambaye alitoa kiasi cha milioni 200 kama mchango wake. Rostam hapo kabla alikiri kuwa yeye ni shabiki wa Yanga, hivyo ikamfungua kuhusishwa na ufadhili wa klabu hiyo yenye makazi yake Jangwani.
Baadae baada ya mahojiano, Rostam Aziz alisema yeye haamini kutumia njia ya mtu mmoja kumiliki timu (Mfano Mo Dewji na klabu ya Simba SC). Mtazamo wa Rostam ni kuwa timu kama Yanga inahitaji nguvu za wanachama, na yeye kupitia kampuni zake anaweza kudhamini ila sio kufadhili. Hapa maanake biashara inaingia.
Hebu tuangalie ni vipi timu yoyote ile ambayo ipo Ligi Kuu Tanzania bara inavyoweza kutengeneza pesa. Timu hizi zote kwa wakati tofauti zinategemea: Mapato ya Mlangoni, Ada za Wanachama, Zawadi za Mashindano, Michango ya Wafadhili na Wadau, Udhamini, Mauzo ya Jezi na Vitu vyenye nembo ya timu. Kila timu ikijaribu kupigana na kimojawapo au vyote ili kujiongezea kipato.
–Wadaau wa Lipuli walianzisha mchakato wa kuichangia timu ipate basi lao la Timu
Mfano, hivi karibuni wadau wa Lipuli FC kutoka Iringa walitengeneza ripoti yao ya kuichangia timu yao Maji ya kunywa, RIPOTI YA MAJI iliyoandaliwa na Danny Manjiwa na Robert Kisinini. Ripoti yao ilieleza wazi idadi ya mechi walizochangia na wastani wa michango hiyo. Jumla ya mechi 40 wadau hao walichangia maji, ikiwa ni mechi za Ligi Kuu (35) na FA (5), ikiwa ni jumla ya shilingi 3,397,200 wastani wa shilingi 84,930 na wastani wa katoni 36 kila mechi. Ripoti pia ilionyesha makusanyo ya mechi za nyumbani (mechi 21, shilingi 1,991,800) na Ugenini ( Mechi 19, Shilingi 1,405, 400). Huu ni mfano wa misaada ya wadau kwa timu yoyote ile.
Ukiangalia hapo tayari michango hii inaweza zaa udhamini kwa timu kama Lipuli kwa kuangalia tu mahitaji yake “Tumependekeza katika ripoti hii uongozi wa Lipuli ukutane na kiwanda cha maji cha Mkwawa, ili wawauzie maji moja kwa moja kutoka kiwandani” Danny Manjiwa. Hii moja kwamoja inamaanisha gharama inaweza kupungua na yawezekana wadau hawa pesa yao ikaenda kufanya kitu kingine.
Kila timu inautaratibu wake wa kupata michango hii mbalimbali. Msimu uliopita yawezekana ni Simba Sc pekee ndio amefanikiwa kwenye makusanyo ya pesa katika Mashindano na Udhamini. Hii ukiondoa michango ya wanachama wake kama walitoa pesa au la, Tazama picha hii hapa chini.
Vilabu vyote vipo ligi kuu kwaajili sio ya kucheza tu nakuwafurashisha mashabiki, vinatakiwa kuangalia mwisho wa msimu vinatengeneza nini. Na kama ingewezekana mapato na matumizi ya vilabu vyote yasisitizwe zaidi kuwekwa wazi sio kwa wanachama tu, hadi kwa wadau wote. Ligi ya Mabingwa, Udhamini wa Sportpesa, Udhamini wa MO Energy na Haki za matangazo, zimempa Simba Sc kiasi cha shilingi Bilioni 5. Bilioni 5 hii haijaangaliwa mapato ya mlangoni na michango ya wadau mbalimbali. Kumbuka haya ni mapato, si faida.
Wategemewe wanachama katika kuendesha timu?
Vilabu vingi hapa nchini vinaendeshwa na katiba zao, ambazo zinawatambua wanachama kama ndio nguzo muhimu ya kufanya maamuzi na mabadiliko katika vilabu hivyo. Ukiondoa vilabu vinavyomilikiwa na taasisi au makampuni vinaweza kuwa na utaratibu wao pekee. “Kwa mtazamo wangu, Yanga haitakiwi kumilikiwa na mtu binafsi wala kutegemea ufadhili kwa sababu ni klabu yenye wanachama na mashabiki wengi“, Rostam Aziz.
Simba na Yanga ni klabu mfano wa ukubwa na mafanikio kwa soka letu. Simba kwa mwaka inaweza kutengeneza Milioni 144 tu kutoka kwa wanachama hai 12,000 huku Yanga ikitengeneza milioni 40 tu kutoka kwa wanachama 2,500. Wanachama wananguvu ya kufanya mabadiliko ya katika yao au jambo lolote lile katika uendeshwaji wa klabu yao. Swali, ni kweli vilabu hivi havihitaji ufadhili au mtu binafsi? na ni kweli wanachama wanaweza endesha klabu? Hatuwezi wakimbia wafadhili, Wadau na Wadhamini katika uendeshwaji wa vilabu hivi.
Klabu labda zinaweza pia boresha jinsi wanavyowasajili hawa wanachama au mashabiki. Mfano, kwa sasa Yanga na Simba zote zina ada moja kwa mwaka, wanatofautiana katika gharama za mwanzo wakati wa kuanza kupata kadi, ambayo kwa Upande wa Simba ipo juu zaidi (18,000/= kupata kadi na 12,000/- ada ya mwaka, jumla 30,000/=) na Yanga fomu inalipiwa 2,000 na ada ni 12,000, jumla 14,000/=.
Hakuna kitu tunaweza boresha hapo kwa lengo la kupunguza utegemezi? “Kuwe na 1,000/= na 100,000/= halafu wa 1,000/= wachague wawakilishi na wa 100,000= wachague wawakilishi kuingia mkutano mkuu” mdau mmoja aliiambia Kandanda akiangalia katika suala la ada kwa mwezi la wanachama na nani aingie katika mkutano mkuu wa wanachama.
Hebu tutumie mfano wa katika picha hii hapo juu, Kwanini vilabu hivi vikawa na utaratibu wa kuwaweka wanachama wao kwa madaraja? Na kila daraja likawa na mkutano wao pekee kwaajili ya kuchagua tu wawakilishi ambao wataingia katika mkutano mkuu. Wanachama hawa katika mkutano mkuu wote watakuwa na kura moja sawa ya maamuzi. Kiwango kwa kila timu inaweza kuamua walipie kiasi gani katika kila ngazi, watatofautiana kwenye vitu vingine tu vya kiuongozi au kuwakilisha klabu tu labda. Inaweza tumia utaratibu huo huo kuwafanya wanachama au mashabiki kuwa na uwezo wa kuingia katika mechi zote za klabu msimu mzima kwa madaraja husika, kupata kalenda, jezi na hata kupata nafasi ya kusafiri na timu bure pindi ikiwa inaenda sehemu.
Haya ni mapendekezo, klabu itatengeneza pesa kutoka kwa madaraja haya, na itaweza kujiendesha na kuwekeza zaidi. Na inaweza fanya kuwa mapato haya yanaweza kuwa yakaenda katika kujenga miundombinu ya klabu ili itengeneze pesa zaidi. Wafadhili na Wadau hawaepukiki, ila kwa utaratibu maalumu unaotambulika, hivyo hivyo kwa wadhamini wa Vilabu.
Imeandaliwa na timu nzima ya waandishi wa Kandanda.co.tz