Vilabu vya Simba na Yanga wajarudi tena dimbani mwishoni mwa wiki hii kuendelea na michezo ya Ligi Kuu ya NBC kama ambavyo ratiba inaonyesha wakiwa na mchezo mmoja pekee wa Ligi mwezi Machi.
Baada ya kumaliza majukumu ya Kimataifa katika michezo ya Klabu bingwa kwa upande wa Simba na Shirikisho kwa Yanga na kupata ushindi sasa wanarudi dimbani katika Ligi Kuu ya NBC.
Simba watakua ugenini kuvaa na Mtibwa Sugar katikati mwa mashamba ya miwa katika Dimba la Manungu mchezo ambao utapigwa saa kumi kamili jioni siku ya kesho Jumamosi. Katika mchezo wa raundi ya kwanza Simba walikua nyumbani na wakafanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao matano kwa sifuri.
Wenyeji Mtibwa Sugar wanashika nafasi ya tisa wakiwa na alama zao 29 wakati wageni wao Simba wapo nafasi ya pili wakiwa na alama 54 nyuma ya vinara Yanga. Mara ya mwisho wawili hao kukutana Manungu mchezo uliisha kwa suluhu.
Yanga wao watakua nyumbani katika uwanja wa Azam Complex kuwakaribisha Geita Gold siku ya Jumapili katika mchezo ambao utapigwa saa moja usiku. Katika mchezo wa mwanzo Geita alipoteza bao moja bila alipokua nyumbani.
Yanga ndio kinara wa Ligi wakiwa na alama 62 wakati kwa upande wa Geita wao wanashika nafasi ya tano wakiwa na alama 34 mpaka sasa.
Yanga wanaingia katika mchezo huo wakiwa na morali ya hali ya juu baada yakupata ushindi muhimu na mnono katika mchezo wa Kiamataifa dhidi ya Real Bamako.
Wananchi bado wapo kileleni huku wakiendelea kupiga hesabu zao vyema za ubingwa na mchezo huo dhidi ya Geita ni wazi watautumia kuendeleza moto wao katika kukusanya alama tatu kuelekea safari yao ya ubingwa mara mbilo mfululizo.