Ameandika Ibrahim Mkamba mwana Yanga kindaki ndaki (Kama ilivyonukuliwa katika mitandao ya kijamii, mtandao wa kandanda.co.tz umeichukua kama ilivyo na kukuwekea hapa)
ACHANA na vitu vya kivyetuvyetu vya ajabu ajabu vya soka ambavyo atakayebainika kuvitenda huchukuliwa hatua na akichukuliwa hatua atazomewa yeye wakati wote tunavifanya, timu kubwa inaweza kujiteremsha bila yenyewe kujua kwa matendo yake.
Simba wanajitahidi kujipa ukubwa kwa hulka yao ya kutoyapa uzito mambo kadhaa wanayostahili kusifiwa. Walibeba ubingwa wa Tanzania Bara wakiwa nje ya Dar es Salaam. Walipofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, walipokewa bila shamra shamra. Kocha wao wa wakati huo alizuia sherehe akisema timu ilikuwa na jukumu zito la mechi za ligi ya mabingwa Afrika na hivyo walipitiliza moja kwa moja kambini. Huo ni ukubwa.
Simba wanapokuwa ndani ya 20 bora Afrika, wanapotoa mfungaji wa bao bora Afrika na wanapoingia robo fainali mashindano ya Afrika mara kadhaa, hawafanyi tafrija yoyote kupongezana. Kwao, hayo ni matukio tu ya kawaida ya kisoka. Msimu ule walipotolewa kwenye mashindano ya ligi ya mabingwa na Jwaneng Galaxy, waliudhika kiasi cha kumfukuza kocha. Hawakufurahi kwenda mashindano ya Shirikisho.
Walipofuzu kuingia makundi ya mashindano hayo, walinuna. Wao ni wakubwa wakajiona wameshuka chini. Wakashiriki hatua ya makundi na kuingia robo fainali bila shangwe.
Wakati walipopangwa kupambana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwenye robo fainali hiyo, wengi tuliamini wangetupwa nje ya mashindano kwa ‘aggregate’ kubwa (idadi kubwa ya jumla ya magoli) kwa sababu mbili. Kwa upande mmoja, Pirates iliaminika kuwa moja ya timu kubwa mno za Afrika na upande wa pili, Simba ya msimu ule ilielezewa kuwa moja ya Simba mbovu mno kuwahi kutokea kwa miaka ya karibuni.
Kilichotokea, walitolewa kwa penalti tano tano baada ya kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake. Tulichosikia ni Simba kusikitika kutolewa mashindanoni. Hatukusikia wakitamba kutolewa kwa penalti tano tano na moja ya timu kubwa za Afrika. Unajua kwa nini? Kwa sababu Simba wanaamini wao ni wakubwa kuliko Pirates ikizingatiwa ushahidi wa kitakwimu unaonesha hivyo.
Ni jana tu nilipofuatilia mahojiano fulani YouTube ndipo nilipojua Simba msimu huu kuanzia hatua ya awali mpaka mzunguko wa kwanza ligi ya mabingwa Afrika walicheza mechi nne ugenini na nyumbani na wakashinda mechi zote nne wakifunga mabao tisa na kufungwa moja tu! Sikulijua hilo kwa sababu Simba hawakutambia matokeo hayo. Huu ni ukubwa.
Kitu pekee nilichokijua wakati ule ni kwa Simba kuingia hatua ya makundi ligi ya mabingwa bila shamrashamra zozote ikitafsirika kuwa kwa ukubwa wao, hatua hiyo ni ndogo na wameizoea.
Kisaikolojia, ukijijenga kuwa mtu wa kufanikisha makubwa, mambo yako ya kukupeleka kwenye hayo makubwa yatafanikiwa na ukijishusha kwa kufanya matendo ya kutafsirika kwamba wewe ni mdogo, utagota mahali kimafanikio na hutaenda juu. Unajua kwa nini? Kufurahia sana mambo ya kawaida na madogo madogo kunakufanya ujione tayari uko juu na hutafikiri kwenda juu. Juu wapi tena zaidi ya hapo?
Kufanya mambo ambayo watu wanayaona makubwa lakini wewe unayaona bado madogo na huyasherehekei kunakufanya utafute makubwa ya kukufanya usherehekee kwani unajiona bado hujafika juu. Simba wako hivyo. Naamini tuna la kujifunza kwa hoja zilizotolewa hapa.