Simba baada ya kumalizana na mtani wake Yanga jumamosi hii anakibarua kingine mkoani Lindi dhidi ya Namungo katika Ligi Kuu ya NBC.
Si mechi nyepesi kama wengine wanavyoweza kudhani binafsi naiangalia kwa utofauti mkubwa, kwa sababu katika timu zenye dhana kubwa ya “professionalism” nchini ni pamoja Namungo FC.
Kuanzia sajili zao, benchi la ufundi, kambi zao na uendeshaji wa klabu kiujumla pamoja na wadhamini.
Ukitoa Simba, Yanga na Azam naamini timu inayofuata kwa kuratibiwa kisasa ni hii, matokeo yake tuliyaona miaka miwili nyuma ilipowakilisha kimataifa hadi ngazi ya makundi japo ilikwenda kuzidiwa huku mbele.
Benchi lake la ufundi linajengwa na kocha mkuu Janza Honour raia wa Zambia anaeaminika kwa kuwa na maarifa (Taaluma) ya juu kwenye mchezo husika lakini anasaidiwa na Kocha mwenye maneno mengi kaka yangu Julio Alberto Pereirra Talantin ambaye pia ni mchezaji na kocha wa zamani wa Simba.
Julio siku zote huwa anaamini yeye ni bora kuliko hawa makocha wa kigeni wanaokuja kufanya kazi na hizi timu.
Hivyo basi kwa kupitia dhana hiyo ndiyo naiona mechi hii kwenda kuwa ngumu sana na najua katika mpira wa miguu unafundishwa ama wachezaji wanaandaliwa kwenye maeneo matatu, kiufundi, kimbinu na kisaikolojia.
Kwa Kaka yangu Julio kwenye maeneo hayo yote huko bora japo siku hizi kwenye eneo la utimamu wa mwili (fitness) kuna makocha maalum, sasa basi hayo maeneo mawili yanayobaki naomba nikuambie kaka yangu ndiyo “Master” hasa hili la ujenzi wa saikolojia.
Julio ni fundi sana kuwakamulia ndimu wachezaji kuwatia ghadhabu ya kuchukua alama 3 toka kwa mpinzani, anaweza kukujasirisha hata kama kwa macho ya kawaida unaona hili haliwezekani.
Kwenye kikosi anajivunia wachezaji wenye uzoefu sana na uzoefu wa kati lakini kila aliyomo kwenye kikosi chake hapungui miaka 4-6 katika uwepo wake kwenye Ligi Kuu au daraja la hivi kwa mataifa mengine.
Kuna Reliant Lusajo ambaye aliuanza msimu vizuri sana lakini sijui kafikwa na nini ana zaidi ya mechi 10 hajafunga, Obray Chirwa naye upepo si mzuri kwenye uwezo wa kufunga hali kadhalika Molinga Falcao bado hajafanya lolote kubwa hadi sasa.
Kwa upande wa Simba Sports naona wana kazi kubwa ya kurejesha form yao na “atmosphere” ndani ya timu kwa kupata matokeo mazuri leo.
Wametolewa kwenye michuano ya kombe la Shirikisho lazima hawatakuwa vizuri kisaikolojia wameshindwa kupata matokeo kwa mtani wao Yanga. Kwa mtizamo huu Simba ni analazimika kufanya juhudi za kushinda huu mchezo na mingine iliyobaki.
Baada ya kuthibitika kwamba Tanzania itaingiza timu nne kwenye mashindano ya CAF kumechochea sana ushindani pia wa nne bora ukiachilia mbali mgao wa Azam kadri ya nafasi uliyomaliza (Coefficients) katika msimamo wa Ligi.
Kwa jicho jingine Kocha Pablo kama vile hayuko sehemu salama baada ya kushindwa kutimiza malengo ya club kwenye ushiriki wa kimataifa, kushindwa kumfunga mtani huenda analimbikiziwa visanga ili apewe mkono wa kwaheri, sasa basi endapo atapoteza mchezo huu anaweza kuunganishiwa “dot”.
Benchi la Simba litambue linacheza mchezo mgumu usio wa lelemama kama nilivyotangulia kueleza japo hivyo basi uteuzi wa kikosi ukategemee mahitaji ya timu.
Namungo mara nyingi wanacheza 4-4-2 hivyo huwenda kikosi chao kikawa na 1 .David Kisu 2 Haruna Shamte 3 Emmanuel Charles 4 .Abdoul Malik 5. Frank Magingi 6. Jacob Masawe 7 Hashimu Manyanya 8 Lucas Kikoti 9 David Molinga 10 Reliant Lusajo na 11 Ramadhani Kichuya.
Simba ni waumini wa 4-2-3-1 hivyo basi
1.Aishi Manula 2 Shomari Kapombe 3 Mohamed Tshabalala 4 Joash Onyango 5 Henock Inonga 6.Jonas Mkude 7 Sakho 8 Kanoute 9 Mugalu 10 Bwalya 11 Morrison.