Ligi Kuu ya Wanawake inafikia tamati leo Jumatano May 17 ambapo mchuano mkali wa kuwania ubingwa huo upo kati ya vigogo wawili Simba Queens na JKT Queens.
Mpaka sasa timu zote zimeshashuka dimbani mara 17 huku JKT Queens wakiwa vinara na alama 43 na Simba wakishika nafasi ya pili wakiwa na alama 42, kila timu imebakisha mchezo mmoja pekee ili kumalizika kwa Ligi hiyo.
Wote wawili Simba na JKT Queens watamalizia michezo yao wakiwa ugenini mkoani Iringa, Simba watakua wageni wa Ceasiaa Queens katika uwanja wa Chuo kikuu cha Mkwawa wakati JKT Queens pia watakua wageni wa Mkwawa Queens katika mchezo utakaopigwa katika uwanja mkongwe wa Samora.
Simba Queens wao wakihitaji ushindi huku pia wakiwaombea mabaya JKT Queens wafungwe ama wapate sare katika mchezo huo ili waweze kutetea ubingwa wao na kuweza kupata nafasi yakwenda kucheza michuano ya kimataifa.
Kwa upande wa JKT Queens wao ni ushindi pekee bila kujali matokea ya timu nyingine na endapo watapata ushindi leo maana yake watakwenda kuiwakilisha nchi katika michuano ya Wanawake ya Cecafa ili kumpata mwakilishi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Endapo watanyakua ubingwa huo maana yake watakua wamewalipa kaka zao wa JKT Tanzania ambao wametwaa ubingwa wa Ligi ya Champioship na kurudi Ligi Kuu.
Michezo mingine ya Ligi hiyo leo ni kati ya Alliance Girs dhidi ya Baobab Queens, Fountaine Gate Princess dhdi ya The Tiger Queens na Amani Queens dhidi ya Yanga Princess. Michezo yote hiyo itaanza muda mmoja ambao ni saa tisa na nusu alasiri.