Karata ambayo alitaka kuicheza Kylian Mbappe mwaka jana dhidi ya Real Madrid ilikuwa bora sana kwake lakini hakufanya hivyo? Mwisho wake hana furaha tena pale Paris na anahitaji kuondoka.
Alex’s Sanchez naye amewahi kucheza karata ambayo haikuwa bora sana kwake, alienda Man United kufata pesa na kuacha pesa ya Man City pamoja na “Project” ya Pep Guardiola ambayo ilimuhitaji pale Etihad.
Eden Hazard naye alicheza karata ambayo imempa wakati mgumu sana baada ya kufika Real Madrid majeraha yamekuwa rafiki kwake na yeye amekuwa rafiki wa benchi pale Santiago Bernabeu, hana simulizi bora tena kama ilivyokuwa pale Stamford Bridge.
Kwanini nimeanza na mifano ya wachezaji hao watatu? Rahisi,leo nipo hapa kuwakumbusha kuhusu Victorian Adebayor ambaye aliacha karata ya Simba SC na akafunua karata ya RS Berkane! Ndio, ilikuwa nzuri kwake lakini imekuwa tofauti kama alivyotarajia.
Sio Adebayor yule ambaye aliimbwa na mashabiki wa Simba pale Benjamin Mkapa Stadium sio yule ambaye aliisumbua Simba kwenye mchezo ule wa CAF pale Nchini kwao NIger.
Simba waliwasilisha ofa yao kwake na makubaliano ya awali yalikamilika kuelekea dirisha kubwa la usajili lakini muda ulipofika kila kitu kikaenda tofauti baada tu ya RS Berkane kuweka mkoni wao pale.
Vizuri! Viongozi wa Simba walifanya kila kitu kilichokuwa ndani ya uwezo wa Klabu ila ofa ya Berkane ilimvutia sana Adebayor! Nzuri zaidi viongozi wa Simba wamewahi kukiri hadharani kwenye baadhi ya mahojiano yao na Waandishi wa Habari.
Familia kubwa ya Simba iliumia kumkosa Adebayor ambaye maslahi ndio yalikuwa kipaumbele kwake, Simba wakasahau kuhusu hili na likapita! Klabu ikaingia sokoni kutafuta machaguzi nyingine.
Adebayor tangu ameenda RS Berkane hana nyakati nzuri sana kama ilivyokuwa nyuma! Leo hii anahesabika amefeli na tetesi zinaeleza huenda akaelekea Amazulu FC.
Kijana amepata fedha nzuri lakini hana furaha tena pale, sisemi kama ilikuwa karata mbaya kwake, hapana ilikuwa nzuri lakini mazingira yamekuwa tofauti kwake.
Kwa sasa sidhani kama Simba inamuhitaji sana Victorian Adebayor kama ambavyo yeye anaihitaji, ndio maisha! Hii ni simulizi yenye funzo kubwa sana kwa wachezaji wetu!.