Ligi Kuu ya NBC Bara inaendelea tena kama kawaidaa baada ya mwisho wa mwisho wa wiki kushuhudia wababe wa nchi wakionyeshana kazi katika Dimba la Benjamin Mkapa.
Baada ya mchezo huo kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana na kufanya Yanga iendelee kubaki kileleni huku wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja, sasa vigogo hao watapisha mikoa ili kuendelea na michezo mingine ya NBC Premier League.
Simba atakua na kibarua dhidi ya Namungo katika Dimba Ilulu mkoani Lindi ambapo katika mchezo wa raundi ya kwanza Simba waliibuka na ushindi dhidi ya Kagera shukrani kwa bao la dakika za jioni kabisa la Medie Kagere.
Namungo inaikaribisha Simba ikiwa nafasi ya 3 wakiwa na alama 29 katika michezo 21 waliyoshuka dimbani wakitofautiana magoli ya kufunga na kufungwa na Azam Fc.
Kwa upande wa Yanga wao watakua ugenini wakikutana na Ruvu Shooting katika Dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma. Ruvu Shooting wameuchagua uwanja wa Lake Tanganyika kama uwanja wao wa nyumbani wakitimiza kanuni ya Bodi ya Ligi inayoiruhu timu kuchagua uwanja tofauti na wa nyumbani katika michezo miwili.
Ruvu Shooting inashika nafasi ya 14 wakiwa na alama 21 wataimaribisha Yanga iliyo kinara wakiwa na alama 55. Mara ya mwisho Yanga kucheza katika uwanja huo walipata kipigo katika mchezo wa Fainali ya kombe la FA.