Baada ya mchezo wa robo fainali ya kwanza kumalizika kati ya Simba na Orlando Pirates na Mnyama kuibuka na ushindi kocha mkuu wa klabu ya Orlando alilalamikia mapokezi na huduma mbovu kutoka kwa wenyeji wao Simba.
Kocha wa Orlando Mandla Ncikazi baada ya mchezo kumalizika alionekana kutoa lawama za wazi kwa Simba na kwa pande zote nje na ndani ya uwanja.
Mtendaji mkuu wa klabu ya Simba Barbar Gonzalez ameonekana kusikitishwa na kauli hiyo ya kocha mkuu wa Pirates na kuahidi kuchukua dhidi yake.
“Lakini kwa mtu kwenda mbali na kusema Simba ilikuwa na lugha mbaya au haikuwapa msaada na ilikuwa na uhasama, haikuwa sahihi kabisa.”
Barbar alikwenda mbali zaidi na kusema hawatoyaacha malalamiko haya hivihivi na kuahidi kuyachukulia hatua zaidi. Huku pia akisema Orlando wanajaribu kucheza na saikolojia yao.
“Sapoti yote iliyotakiwa ilitolewa na Simba haijawahi kuwa mwenyeji mbaya. Tunataka kupeleka jambo hili mbele zaidi. Nataka kutumia hili kama mfano kwa wengine.
“Kuna watu unaweza kuhangaika nao na kujaribu kucheza nao baadhi ya michezo ya kisaikolojia na ninaelewa kuna hofu juu ya usalama wa kazi kwa upande wake na benchi la ufundi la Orlando Pirates. Lakini hii sio njia sahihi ya kuokoa kazi zao na hii sio njia sahihi ya kuzungumza juu ya kila mmoja.” Barbar Gonzalez.
Mtendaji huyo pia hakusita kuonyesha hofu yake kuelekea safari yao ya Afrika Kusini na kusema waziwazi hali ya usalama jinsi ilivyo nchini humo.
“Pia inaleta hofu kubwa kuelekea Afrika Kusini, tunajua kuna uhalifu mkubwa na tunaelewa changamoto zinazowakabili wananchi wa Afrika Kusini kwa sasa hivyo unaanza kuhoji aina ya mapokezi ambayo unaweza kupata au kutokupata, Nina wasiwasi sana juu ya hili.” Barbar aliongeza.
Orlando Pirates wanatarajiwa kuwakaribisha Simba SC kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa robo fainali ya michuano hiyo utakaopigwa Jumapili Uwanja wa Orlando. Ambapo katika mchezo wa kwanza Simba waliobuka kinara kwa bao moja bila la Shomary Kapombe katika Uwanja wa Mkapa.
Mshindi Simba wanahitaji sare ya aina yoyote ile ili waweze kulinda ushindi wao wa bao moja bila na kwenda hatua inayofuata ya nusu fainali.
Chanzo kickoff magazine.