Wekundu wa Msimbazi Simba wanashuka dimbani leo majira ya saa kumi jioni Benjamin Mkapa kuwavaa Wydad Casablanca katika robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakitafuta rekodi yao wenyewe ya mwaka 2003.
Simba wanakwenda kukutana na Wydad ambao ndio bingwa mtetezi wa kombe hili baada ya mwaka jana kumfunga Al Ahly katika fainali lakini kibaya kwao hawatakua na mlinda mlango wao namba moja Aishi Manula.
Tayari Simba kupitia msemaji wake Ahmed Ally walishasema wanataka kuwatoa mabingwa watetezi Wydad kama ambavyo walifanya mwaka 2003 walipowatoa Zamalek ya Misri. Na sasa Simba wanapaswa kuiota ndoto hiyo bila askari wake namba moja Aishi Manula.
Manula aliumia bega katika mchezo wa robo fainali ya kombe la FA dhidi ya Ihefu na hivyo kukaa nje kwa wiki mbili sasa akizikosa mechi mbili dhidi ya Ihefu na ile ya watani Yanga ambazo zote mbili Ally Salim kipa namba tatu alikaa langoni.
Kipa namba mbili wa Simba ambae yupo katika kiwango kizuri Benno Kakolanya amekosa imani mbele ya viongozi wa Simba baada ya kusemekana tayari amemalizana na Singida Big Stars na hivyo kupekea kukosa hata ule mchezo wa Watani na langoni akakaa Salim ambae ni namba tatu.
Pasi na shaka kiwango kizuri, uzoefu pamoja na uongozi mzuri alivyonavyo Aishi Manula ilipaswa kuwa silaha namba moja ya Simba katika kutafuta kuishi ndoto zao mbele ya Wydad Casablanca lakini kutokana na majeruhi hatokuepo hivyo Simba wataingia uwanjani bila yeye.
Ni wazi sasa langoni atakaa Ally Salim ama Benno Kakolanya katika kuifanikisha Simba kuishi ndoto zake, katika mchezo wa mwaka 2003 langoni alikaa Juma Kaseja na kwa ujasiri mkubwa aliivusha Simba kwa kudaka mikwaju ya penati baada ya matokeo ya sare kwa michezo yote miwili hivyo basi ni Benno ama Salim atapaswa kuvaa viatu vya Manula akiwa na ujasiri wa Kaseja katika kuivusha Simba mbele ya bingwa mtetezi Wydad.
Ama kwa hakika yoyote atakaeanza lango iwe ni Ally Salim au Benno Kakolanya atapaswa afahamu amebeba ndoto za Wanasimba katika mikono yake hivyo ni wakati wake kutumia mikono yake kuliweka lango la Simba salama mbele ya Waarabu hao.