Sambaza....

Karibu katika makala maalumu za klabu Bingwa Barani Afrika. Tovuti hii itakuletea mfululizo wa makala hizi hasa kuziangazia timu zote wapinzani wa timu ya Simba SC kutoka hapa hapa nyumbani “TANZANIA”.

Lengo hasa ni kuwajua wapinzani wa mabingwa hao wa Tanzania bara msimu 2017/18 katika hatua hii ya makundi ambapo Simba imepangwa katika kundi D. Kundi hili linahusisha timu nne, AS Club Vita, Simba, JS Saoura na Al-Ahly. Huku mechi ya kwanza inatarajiwa kuchezwa January 11, Huku Simba Sc ikianzia nyumbani kukwaana na  JS Saoura katika uwanja wa taifa.

Kwa kuanza, Tovuti hii inakuletea undani juu ya klabu ya AS Vita Club ya nchini Congo, kwa kuangazia mafanikio yake kitaifa na kimataifa, takwimu na hali ya kikosi chake kwa sasa.

    AS Vita Club  (Pomboo Weusi).

Association Sportive Vita Club maarufu kwa jina la AS Vita Club ni klabu kutoka Kinshasa, nchini Congo. Klabu hii inayofahamika pia kwa jina la  Pomboo Weusi “Black Dolphin” ilianzishwa mwaka 1935, uwanja wake  unaitwa Stade Des Martyrs, uko katika mji wa Kinshasa, una uwezo wa kuingiza watu 80,000 hii ni zaidi ya uwanja wa taifa wenye uwezo wa kubeba watu 60,000 pekee.

Jina la Klabu hii limebadilishwa mara tatu kabla ya kuitwa AS Vita Club. Mwaka 1935 klabu hii ilianzishwa na kuitwa Renaissance in rue Usoke n’75 mjini Kinshasa. Mwaka 1939 jina hilo lilibadilishwa na kuitwa Diables Rouges, mwaka 1942 likabadilishwa tena na kuitwa Victoria klabu na mara ya mwisho kabisa mwaka 1971 ikabadilishwa na kuwa Vita Club

Rais wa klabu hiyo wa sasa anaitwa Gabriel Amisi Kumba, kocha wake anafahamika kwa jina la Mkongo Florent Ibenge mwenye miaka 57 ambaye alijiunga na klabu hii mwaka 2012 akisaidiwa na Wakongo wenzake wawili, Raoul Shungu na Jean- Kasongo Banza.

Mataji.

AS Club Vita ni miongoni mwa vilabu mashuhuri nchini Congo na Afrika kwa ujumla wake , kwani tayari imeshabeba mataji ya ligi mara 14 katika Ligi kuu nchini Congo inafahamika kwa Linafoot. AS Club Vita imebeba vikombe mwaka 1970, 1971,1972, 1973, 1975,1977,1980, 1988,1993, 1997, 2003, 2010, 2015 na mwaka huu 2018 wamechukua tena taji la ligi.

Katika mshindano ya Afrika, Club Vita ilishawahi kuwa bingwa wa Klabu bingwa Afrika mara moja mwaka  1973, na mwaka huu imefika fainali katika mashindano ya shirikisho Afrika.  Na katika mashindano ya Afrika Mashariki “Kagame Cup” ilishawahi kushika nafasi ya 3 mwaka 2012.

SAFARI YA AS CLUB VITA HADI KUFIKA HATUA HII.

Katika mzunguuko wa kwanza, Club Vita ilicheza mechi mbili dhidi  ya Bantu ya Lesotho, na kuichapa goli 4-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa nchini DRC Congo, katika mechi ya marudiano Club Vita ilifanikiwa kupata sare ya 1-1 ugenini na kuwafanya wavuke hatua ya kwanza na kuingia hatua makundi kwa jumla ya magoli 5-2.

MSIMU ULIOPITA ULIKUWAJE KWA AS CLUB VITA.

Kama kawaida yake, klabu hii ilishiriki mashindano haya makubwa zaidi Afrika kwa ngazi ya Vilabu baada ya kushika nafasi ya pili katika ligi nchini Congo na kuwapatia nafasi ya kucheza mashindano haya.

Kwa nchi kama Congo hupata nafasi ya kuingiza timu mbili katika mashindano haya, hii ni kutokana na viwango vyao katika michuano iliyochini ya Caf kufanya vizuri ndani ya miaka mitano katika ngazi ya vilabu.

As Club Vita ilifuzu katika hatua ya awali ya mchujo kwa kuichapa jumla ya goli 6-1 Mighty Wanderers ya Malawi na kufuzu katika hatua ya kwanza ya mashindano haya. Kipindi hicho Tanzania tukiwakilishwa na Yanga SC, ambayo nayo ilifuzu kwa kuifunga Saint Louis Suns United kwa jumla ya goli 2-1.

Huku Yanga ya Tanzania ikitolewa na  Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya goli 2-1 katika raundi ya kwanza, AS Club Vita nayo ilitolewa na Difaa El Jadidi ya Simon Msuva wa Tanzania kwa jumla ya goli 3-2.

Kutolewa katika hatua hii, kunazifanya timu husika kushushwa mpaka katika mashindano ya Shirikisho barani Afrika. Yanga na AS Club Vita zote zilishushwa katika mashindano hayo. Kipindi Yanga na AS Club Vita zinaingia katika hatua ya mwisho, ili kufuzu hatua ya makundi Shirikisho Afrika , Klabu ya Simba tayari ilikwa tolewa na Al-Masry ya Misri kwa jumla ya goli 2-2, Al- Masry wakifuzu kwa faida ya goli la ugenini hivyo kufanya vilabu hivi kutokutana katika mashindano hayo.

Katika raundi hii ya “play-off” AS club Vita walifuzu kuingia hatua ya makundi kwa kuwakandamiza ndugu zao jumla ya goli 6-1 CS La Mancha ya huko huko Congo. Huku Yanga nayo ikifuzu katika hatua hii kwa kuichapa jumla ya goli 2-1 Welayta Dicha ya Ethiopia.

Katika hatua ya Makundi, AS Club Vita ilifuzu katika hatua hii kwa kushika nafasi ya pili katika kundi A . Kundi A lilikuwa na vilabu kama Raja Casablanca, ASEC Mimosas na Aduana Stars ya Ghana. AS Club Vita ilijikusanyia jumla ya alama 10 chini ya kinara Raja Casablanca na alama zake 11. Hivyo kuzifanya timu hizi mbili za juu kufuzu robo fainali.

Katika hatua ya Robo fainali, AS Club Vita ilipangiwa na RS Berkane na kuichapa jumla ya goli 4-2 na kufanikiwa kufuzu nusu fainali.

Katika hatua ya nusu fainali, ilicheza na  Al-Masry iliyomtoa Simba, na kufanikiwa kuichapa jumla ya goli 4-0, mechi ya kwanza kule Misri wakitoka sare 0-0 na kule Congo Al Masry walikubali kulala kwa goli 4-0.

Hatimaye, AS Club Vita inaingia fainali na kukutana na Raja Casablanca walikuwa katika kundi moja. Kama ilivyo ada ya fainali hizi huchezwa mara mbili yaani nyumbani na ugenini.

Katika fainali ya kwanza iliyochezwa katika uwanja wa Stade Mohammed V, chini ya watazamaji wapatao 45,000 hadi filimbi ya mwisho inapulizwa na mwamuzi, Maguette N’Diaye wa Senegal, Casablanca iliibuka na ushindi wa magoli 3-0 yakiwekwa kimnyani na Rahimi (2) na moja la penati ilikiwekwa na Benhalib.

AS Club Vita ilikuwa na mtihani mkubwa katika fainali ya pili ilichezwa  pale Congo. Mchezo huo ulipigwa pale Stade des Martyrs kukiwa na watazamaji 75,000, na aliyepewa dhamana ya kupuliza filimbi alikuwa ni Victor Gomes kutoka Afrika ya Kusini. AS club Vita ilikuwa ya kwanza kuruhusu goli, Hafidi akiifungia Casablanca dakika ya 21 na kuipa mtihani mzito AS Club Vita.

Mchezo huo ulimalizika kwa Ushindi usio na faida wa goli 3-1, magoli ya Mundele, Batezadio na Ngoma katika dakika za 45+4’,71’ na 74’ mtawalia. Casablanca walibeba ndoo kwa jumla ya goli 4-3.

Jean Marc Makusu , mshambuliaji katika timu ya AS Club Vita.

Katika mshindano hayo, mfungaji bora alitoka katika timu washindi, Casablanca, Mahmoud Benhalib kwa kufunga magoli 12, Wa pili akitokea AS Club Vita, Jean Marc Makusu Mundele akifunga magoli 11 na mwingine ni Fabrice Luamba Ngoma wa AS Club Vita akiwa na goli 4.

HALI YA KIKOSI KWA SASA.

AS Club Vita kama timu ina jumla ya wachezaji 29, wenye wastani wa umri wa miaka 26 kila mmoja. Kati ya kikosi hicho chote, wageni ni watatu pekee. Mwaka huu pekee, AS Club Vita imefanya maingizo mapya ya wachezaji watano, kwanza ni golikipa, Frank Nkela aliyejiunga mwezi januari, Nelson Lukong (golikipa) aliyejiunga mwezi julai mwaka huu, Ngudikama (kiungo) naye amejiunga julai mwaka huu, M.Banga, Tonombe (kiungo mkabaji),Akwo Ayuk (mshambuliaji), Ilunga (mshambuliaji ) na Makusu (Mshambuliaji).

Ujio wa wachezaji hawa umeonekana kuimarisha kikosi hiki.

Kikosi ambacho huwa kinaanza katika mechi nyingi za AS Club Vita huwa kina wachezaji hawa:

MAGOLIKIPA.

1. H.LOMBOTO, 16.  NELSON LUKONG

WALINZI.

  • 12. MONDIA KALONJI
  • 4. Y. BANGALA
  • 3. D. SHABANI
  • 20. BAFOLA DIDO
  • 13. LUZOLO SITA.
  • 14.NGONDA MUZINGA
  • 26. MAKWEKWE KUPA

VIUNGO.

  • 8. L. NGOMA
  • 5. E. EMOMO
  • 6.MUNGANGA
  • 24. MANI

WASHAMBULIAJI.

  • 2. EMMANUEL NGUDIKAMA.
  • 21. D. MOLOKO
  • 7. MUKOKO BATEZADIO.
  • 29. JEAN-MARC MAKUSU

Wachezaji wako wengi katika kikosi hiki lakini hao ndio huwa waanza mara kwa mara.

Simba SC inatarajiwa kukutana na AS Club Vita tarehe januari 18 mwaka 2019 ikiwa ugenini baada ya mechi ya kwanza nyumbani Dar Es Salaam dhidi ya Js Saoura ya Algeria kabla ya kurudiana na As Vita machi 15 katika uwanja wa Taifa, Dar Es Salaam.

Sambaza....