Kama ambavyo kuna Simba Day ile siku ya tarehe nane mwezi wa nane ndivyo sasa ilivyo ni Simba wiki, na hii ni kutokana na matokeo ya Simba mbele ya JS Saoura na kinachohitajika mbele ya AS Vita.
Ndio ni Simba wiki ambayo ilifunguliwa siku ya Jumatatu na msemaji wa klabu ya Simba ndugu Hajji Manara alipokua makao makuu ya klabu ya Simba pale Msimbazi Kkoo alipokua anaongea na waandishi wa habari. Na hapa ndipo ilipokuja ile kauli mbiu ya “DO or DIE”. Kila Mtanzania, vyombo vya habari, vijiwe vya kahawa na maofisini mzungumzo ni mchezo wa Simba tu dhidi ya AS Vita ambao utaamua hatma ya Simba na Taifa kwa ujumla kuelekea robo fainali ya Klabu Bingwa Africa.
Kuelekea mchezo wenyewe Simba itamkosa Jonas Mkude huku Haruna Niyonzima na Pascal Wawa wakiwa kwenye hatihati kutokana na majeruhi. Lakini habari njema ni urejeo wa Emmanuel Okwi na Juuko Mursheed ambao waliukosa mchezo wa Algeria dhidi ya Saoura.
Klabu ya Simba imezoelekea kupata matokeo katika mechi ngumu na hii ni kutokana na wachezaji wazoefu haswa katika safu ya ushambuliaji. Emmanuel Okwi, John Bocco, Meddie Kagere na hata Cleotus Chama hawa ndio wamekua wachezaji pekee wanaoibeba Simba katika michezo migumu. Rejea katika michezo migumu dhidi ya Nkana, Al-Ahly, JS Saoura na Yanga pale uwanja wa Taifa utaona ni hao pekee wamekua wakiimbwa na mashabiki baada ya mchezo kumalizika.
Kuelekea mchezo dhidi ya Vita ni wazi majina ya nyota hao tayari yapo mikononi kwa Florent Ibenge na Rayol Shungu (Wakuu wa benchi la ufundi la As Vita). Hivyo haitoshangaza wachezaji hao wakiwekewa ulinzi maalum ili wasilete mazara langoni mwao.
Lakini sasa ni zamu ya wachezaji wengine wasioimbwa sana kutumia nafasi na kuweza kuandika majina yao katika mioyo ya mashabiki wa Simba kwa kufanya mambo makubwa pale Kwa Mkapa siku ya Jumamosi dhidi ya Vita.
Wachezaji kama Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin na Adam Salamba ni wakati sasa wa kutumia nafasi watakayoipata siku ya mchezo na kufanya “Wonders” ili kuweza kuifunga Vita na kufuzu hatua ya robo fainali. Wakati Vita watakua “busy” na Kagere uwanjani ni nafasi kwako Salamba kuweza kufunga goli, Vita wakiwa wanajiandaa kumthibiti Chama ni wakati wa Dilunga kupiga pasi za mwisho kwa kina Bocco na Okwi.
Sio hao tuu lakini kina Wawa na Juuko wakati wa mipira ya adhabu na kona mkivitumia vichwa vyenu kwa ufasaha zaidi huenda mkawa na nafasi mpya ndani ya mioyo ya WanaSimba. Mohamed Hussein na Zana ni vizuri basi mkapiga mitungi yenye macho pale langoni kwa Vita na kuleta mazara kwa “kumwaga maji” yenye kufika kwa walengwa kina Kagere, Bocco au Salamba.
Ni wazi sasa kuanzia mazoezi ya leo jioni pale Bokko Beach kina Dilunga, Niyonzima na Salamba mkayafanya kwa nguvu na malengo ili kumshawishi mwalimu kupata nafasi ya kuishangaza AS Vita pale kwa Mkapa.
Adam Salamba, Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin na Hassan Dilunga Juhudi na kufanya mazoezi kwanguvu kwa siku hizi tatu ndio chanzo cha kwenda kuwa mashujaa wapya siku ya Jumamosi.