Simba watashuka Dimbani kesho kuvaana na Azam Fc katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA utakaopigwa katika uwanja wa Nang’wanda Sijaona mkoani Mtwara majira ya jioni.
Kuelekea mchezo huo wa nusu fainali kocha msaidizi wa Simba Juma Mgunda amesema “Maandalizi ya mchezo yamekamilika, wachezaji wapo kwenye hali nzuri. Tunajua utakuwa mchezo mgumu, Azam ni timu nzuri na tunaiheshimu.”
Pia Mgunda alikiri walipoteza mchezo wa Ligi raundi ya kwanza na kutoka sare wapili lakini amesema huu ni mchezo watofauti na una mbinu tofauti.
Juma Mgunda “Katika mechi za ligi msimu huu wamefanya vizuri dhidi yetu lakini mchezo wa kesho ni tofauti na mtoano kwahiyo hata mbinu zitakuwa tofauti, tumejipanga kwa ajili ya kupata ushindi.”
Nahodha Mohamed Hussein akiongea kwa niaba ya wachezaji wenzake amesema kwao mchezo wa kesho ndio tumaini pekee kwani wanalihitaji taji hilo.
“Matumaini yetu yamebaki zaidi kwenye michuano hii, tunajua ugumu na umuhimu wa mchezo lakini tupo tayari kupambana kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Mohamed Hussein.
Mara ya mwisho Azam na Simba kukutana katika michuano hiyo walikutana katika nusu fainali msimu wa 2020/2021 na Simba aliibuka na ushindi wa bao moja bila likifungwa na Luis Miquissone.