Msimu mpya ushaanza. Lakini moja ya kitu ambacho kilikuwa kikubwa sana hapa nchini ni matamasha ya Simba Day , Azam Festival na Wiki ya wananchi.
Ni matamasha ambayo yalishika hisia kubwa sana hapa nchini na nje ya nchi. Watu wengi waliyaongelea katika mlengo chanya nje na ndani ya nchi yetu.
Watu ambao walikuwa nje ya nchi walikuwa wanashangaa kuona kitu kipya ambacho hakijazoeleka kwenye mpira wa miguu duniani.
Kitendo hiki kimeonekana ni njia mpya ya kutangaza bidhaa za mpira wa miguu kwa faida kubwa sana kibiashara.
Matamasha haya yanaonekana yanauhitaji mkubwa ndani na nje ya nchi. Simba , Yanga na Azam FC wanatakiwa kujifunza namna ya kuyapelekea haya matamasha nje ya nchi.
Wanaweza kuanza na nchi moja afu baada ya hapo wakayasambaza kwenye nchi za Afrika Mashariki na kati. Moja ya kitu kizuri ambacho vilabu hivi vitatu vilifanya kwenye matamasha yao ni kuhusiana muziki na mpira kuwa sehemu moja.
Azam FC walimleta Alikiba kwenye tamasha lao , Simba walimleta Diamond Platnumz na Yanga walimleta Harmonize kwenye tamasha lao. Kwa namna moja au nyingine hawa wasanii walihusika kwenye kuhamasisha matamasha haya.
Katika harakati za kuyapelekea nje ya nchi haya matamasha tunatakiwa kuwafikiria hawa wasanii kwenye hizo nchi. Mfano Kenya na Uganda ni wateja Wazuri wa muziki wetu.
Mara nyingi kwenye YouTube wasanii wetu wamekuwa trending number moja kwenye nchi za Kenya na Uganda. Hii ni kuonesha namna ambavyo muziki wetu ulivyo na nguvu.
Na wasanii hawa watatu , Alikiba , Harmonize na Diamond Platnumz wana nguvu sana kwenye hizo nchi. Tunaweza tukaanza na Kenya.
Kukawa na Simba Day au Wiki ya Wananchi au Azam Festival nchini Kenya. Ili kuongeza ushawishi kwenye matamasha haya tunachukua wasanii ambao wana nguvu na kuwatumia nchini Kenya.
Wasanii hawa wakaungana na wasanii baadhi wa Kenya wenye ushawishi kwa ajili ya kutumbuiza. Hii itawasaidia Simba , Yanga na Azam FC kuongeza mashabiki nje ya nchi na kuoanua wigo wao wa kuuza bidhaa zao kama jezi.