Sambaza....

Hivi unamkumbuka Mikel Arteta Amatriain? Achana na  Miguel Arteta, mtengeneza filamu, namaanisha yule  mkata umeme wa Arsenal miaka ya 2011,aliyekata ukame wa vikombe kwa miaka 9 pale kwa washika bunduki wa  Arsenal akicheza kama kiungo mkabaji chini ya Arsene Wenger.

Unajua kwa sasa yuko wapi? Jibu ni jepesi tu, kwa sasa ni kocha msaidizi wa Man city chini Pep Guardiola kama kocha mkuu. Msimu wa 2016/17 ulikuwa ni mgumu sana kwa Guardiola kwani alikuwa mgeni katika ligi ya kuu nchini Uingereza, na hata falsafa zake zilikuwa bado hazikaririki  kwa wachezaji wake. Nakumbuka mechi ya kwanza Gurdiola alipoteza kwa 1-0 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na ligi.

Katika msimu huo, Guardiola hakuibuka na kikombe chochote licha ya kushinda mechi 10 mfululizo katika ligi ikiwemo dhidi ya hasimu wake Jose Mourinho akiwa na Man U, Man city ilitolewa na Monaco katika hatua ya 16 bora, katika mashindano ya klabu bingwa barani ulaya.

Juhudi kubwa alizozifanya Guardiola katika msimu wa 2017/18 ziliungwa mkono na kocha msaidizi, Arteta na kuisaidia Man city kushinda kombe la Calabao baada ya kuichapa Arsenal 3-0 na kubeba kombe la ligi na kuvunja rekodi ya kufikisha alama 100 katika ligi hiyo, na hii ni baada ya kufanya usajili katika eneo la golikipa, Ederson Moraes, na mabeki wa pembeni Benjamin Mendy na Kyle Walker, pia alimsajili Benardo Silver kutoka Monaco na Danilo kutoka Real Madrid.

Pep Guardiola, kocha wa Man City.

Katika kipindi chote hicho cha mabadiliko ya Man City, Arteta kama kocha msaidizi alifanya kazi kubwa ya kupanga mikakati na mbinu za kuinusulu Man City isipitie kipindi kigumu wakati wote wa mabadiliko. Arteta alikuwa ni daraja imara kati ya wachezaji na kocha. Yeye ndiye aliyekuwa akitekeleza maagizo ya kocha mkuu na kufanya shughuli zote za klabu kwa vyombo vya habari kwa mambo yanayomuhusu kocha.

Simba ni miongoni mwa klabu zinazoongozwa bila kocha msaidizi kwa sasa, baada ya kumalizana na aliyekuwa akihudumu nafasi hiyo, Masoud Juma. Unaweza kujiuliza hivi “Kwani kuna athari yoyote ya kutokuwepo kwa kocha msaidizi Simba? Jibu lako lihifadhi kwanza.

Patrick Aussem, kocha mkuu wa Simba SC.

Kwa klabu kama Simba ambayo inamuelekeo wa kuiendesha timu  kisasa, ni lazima iwe na kocha zaidi ya mmoja, kama ilivyo kwa timu kama Man u, ambayo ina kocha wa viungo, na msaidizi na wengine  wabobezi katika Nyanja mbalimbali, na hii huleta ufanisi wa kazi katika klabu. Kocha msaidizi husaidia kusimamia programu za kocha mkuu, kutoa ushauri wakati wa mchezo, na kushika nafasi ya kocha mkuu kukitokea tatizo lolote.

Aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Masoud Juma.

Asaivi Patrick Aussem anafanya kila kitu pekeyake, yeye ndiye kocha mkuu na yeye ndiye msaidizi. Anasaidiwa na watu wasiokuwa na taaluma ya ukocha  na unatarajia mambo mazuri. Hata Aussem angekuwa na uzoefu mkubwa kiasi gani, angehitaji tu kocha msaidizi. Makocha wote waliopita klabuni hapo kama makocha wakuu, walikuwa na  wasaidizi wao, kama ilivyokuwa kwa Joseph Omog na Jackson Mayanja na Masoud Juma, Lecchantre na Masoud.

Wakati Simba wanamtangaza Aussem kama kocha mkuu, walisema wazi kuwa, kocha anahitaji kocha msaidizi mzawa, ili aweze kumpa uzoefu wa kazi, wazo lake lilionekana kuwa zuri kwakuwa anataka ahamishe ujuzi kutoka kwake kwenda kwa mzawa. Lakini Simba walisema Masoud Juma anatosha kuwa kocha msaidizi, baada ya Juma kutimuliwa mbona Simba bado wako kimya? Vipi wameshalisahau wazo la Aussem? Bila kupepesa macho Simba inahitaji kocha msaidizi, ili kuwe na mgawanyo wa majukumu.

Simba kwa sasa ipo katika mshindano mengi yakiwemo yale ya klabu Bingwa Afrika, inahitaji kocha msaidizi mwenye uzoefu na ligi ya ndani na kimataifa. Makocha wasaidizi husaidia masuala ya ushauri wakati wa mechi, kuliko Aussem kupokea ushauri kwa watu wasio na taaluma.

Aussem naye anaogopa nini ? kwanini asiilazimishe klabu itafute kocha msaidizi haraka iwezekavyo? Au atakuwa anamkumbuka Dr.Otto Nerz, aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya  Ujerumani mwaka 1934 na kuifikisha ujerumani katika nafasi ya tatu. Mwaka 1936 Dr Otto alitimuliwa kama kocha mkuu na nafasi yake kuchuliwa na aliyekuwa kocha wake msaidizi, Sepp Herberger baada ya Ujerumani kutolewa katika mchezo wa robo fainali katika mashindano ya kiangazi ya Olimpiki.

Sifikirii katika hilo lakini Simba inahitaji kocha msaidizi mwenye sifa makinifu za kufundisha klabu kama Simba yenye mambo mengi ndani na hata nje ya uwanja.

Sambaza....