SIKU tisa tu bila uwepo wa ‘mwekezaji mtarajiwa’ Mohamed Dewji ‘MO’ klabu ya Simba SC ‘ilitengeneza’ deni lisilopungua Shilingi milioni 70 katika hoteli moja ya kifahari jijini Dar es Salaam. MO alitekwa na kushikiliwa kwa muda wa siku tisa mapema mwezi huu na watu wasiojulikana.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili Zacharia Hans Poppe mara baada ya kuachiwa kwa dhamana aliungana na kaimu Rais wa klabu hiyo, Salim ‘Try Again’ na kulipa deni hilo na mambo yakaendelea kwenda sawa. Lakini sasa siri imevuja wakati huu klabu ikielekea katika uchaguzi wake mkuu Novemba 3 mwaka huu.
“Wakati MO akiwa kizuizini mambo yalianza kwenda hovyo na ndani ya wiki moja tu, klabu ilikuwa ikidaiwa zaidi ya shilingi Milioni 70 kutokana na gharama mbalimbali. Kinachoshangaza wajumbe wa kamati ya utendaji karibia wote walikimbia na kumuacha kaimu Rais pekee akipambana. Bahati nzuri ni kwamba, Salim alimfuata Hans Poppe mara baada ya kuachiwa kwa dhamana na mara moja akalipa pesa hizo” Kimesema chanzo cha habari hii.
Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara wanaelekea katika uchaguzi mkuu wa kupata Rais na wajumbe wa bodi ya ukurugenzi Novemba tatu mwaka huu katika ukumbi wa PTA uliopo katika viwanja vya Sabasaba, Temeke, Dar es Salaam.