SIKU ambayo Azam FC wanatangaza kutoendelea na wachezaji wao kadhaa akiwemo mshambulizi Mzambia, Obrey Chirwa klabu bingwa nchini Simba SC wao walikuwa wakimtangaza mlinzi wa kati Kennedy Juma kutoka Singida United.
Ukiachana na Chirwa-mfungaji wa goli pekee lililoipa Azam FC taji la FA Juni Mosi mwaka huu, wachezaji kiungo mshambulizi wa pembeni, Ramadhani Singano, mlinzi wa kushoto, Hassan Mwasapili, washambuliaji, Daniel Lyanga, Mghana Enock Atta, kiungo mshambulizi, Joseph Kimwaga pia ni miongoni mwa wachezaji ambao hawataendelea kuichezea Azam FC msimu ujao.
Katika utambulisho wa Kennedy, pembeni yake alionekana kiungo mshambulizi, Miraji Athuman ‘Shevchenko’ na kwa taarifa zilizopo ni kwamba, Miraj pia amesaini kuichezea Simba msimu ujao. Kurejea kwake Simba misimu mitano baada ya kuondoka na kuzichezea klabu kama Mwadui FC na Lipuli FC kunamfanya kijana huyo mwenye kipaji kurudi Simba akiwa amepevuka Zaidi kimpira na kiumri.
Baada ya kuichezea klabu hiyo bingwa nchini kwa mafanikio katika kikosi cha vijana ikiwemo kuisaidia timu kubwa kutwaa mataji ya Mapinduzi Cup, Super 8, Miraj aliondolewa katikati ya mwaka 2014 baada ya klabu kuamua kuachana na ‘mradi wao wa vijana’.
Je, usajili huu ni stahili kwa Simba? Ndiyo, kama Miraj mwenyewe ataamua kuendeleza mapambano yake kiuchezaji bila shaka anaweza kuingia katika kikosi cha kwanza hata kama hakuwa akianza mara kwa mara.
Ataisaidia Simba, bila shaka na pengine hii ni nafasi yake nzuri ya kufanya mambo aliyoshindwa kufanya huko nyuma kutokana na uzoefu wake mdogo, lakini kwa ‘jicho la tatu’ huyu si mchezaji wa klabu bingwa Afrika msimu ujao.
Kama ni nyongeza katika ligi na michuano ya ndani sawa, lakini kusema ni mchezaji aliye tayari kubeba majukumu yanayoachwa na Mganda, Emmanuel Okwi, ama kuchukua nafasi anapokosekana nahodha, John Bocco ama Mnyarwanda, Meddie Kagere, hapana. Hata takwimu zake zinamuhukumu, katika ufungaji ama usaidizi wa kupatikana kwa magoli. Simba inapaswa kumsaini Miraji, kumrejesha kikosini, Marcel Kaheza lakini lazima pia wamsaini mchezaji aliyekamilika kwa michuano ya Caf.
Sijashangazwa na Azam FC kuachana na Chirwa baada ya mkataba wake wa miezi sita kumalizika. Mzambia huyo licha ya kufunga goli pekee katika mchezo wa fainali katu hakuwahi kuonyesha jitihada na kujitoa uwanjani- hata siku ya mchezo wa fainali ya FA dhidi ya Lipuli FC.
Chirwa hakuwa hakijitoa Azam FC , hii ni sababu muhimu iliyopelekea klabu hiyo bingwa ya Kagame Cup kugoma kumuongezea mshahara Mzambia huyo. Nashangazwa na Simba kusema wanajenga timu ya ushindani barani Afrika lakini wanamsaini Miraj kama mbadala wa Okwi.