Mshambuliaji wa zamani wa Newcastle United Alan Shearer amesema ligi kuu ya England ni kama ya mafarasi wawili kwa sasa licha ya baadhi ya timu kuendelea kufanya vizuri mpaka sasa mechi nane zikiwa zimeshachezwa.
Shearer amesema ingawa alama ambazo zinawatofautisha timu tano za juu ni alama mbili lakini bado anaziona timu za Liverpool na Manchester City kama timu ambazo zinanafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa msimu.
Amesema timu kama Arsenal, Chelsea na Tottenham zinafanya vizuri kwa sasa lakini bado hazioneshi kama zinaweza kutwaa ubingwa msimu huu, kama ilivyo kwa Liverpool na mabingwa watetezi Manchester City.
“Kuna ushindani kwenye nafasi za juu, alama mbili zinazitofautisha timu tano za juu, lakini nazipa Manchester City na Liverpool nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, Arsenal wameshinda mechi sita mfululizo ni jambo zuri, lakini sioni kama ni timu inayoweza kuleta ushindani na sidhani kama hata nafasi nne za juu wataweza kuingia,” amesema.
“Manchester United mwanzoni niliwapa nafasi wao na Liverpool kuleta changamoto kwa Manchester City lakini kwa sasa nimewatoa kabisa katika nafasi hiyo, Tottenham wao bado hawajapata kiwango kizuri cha ushindani,” Shearer amesema.
Kuhusu Chelsea Shearer amesema ni timu ambayo inaweza kuleta changamoto lakini bado ni timu ya mtu mmoja ambaye ni Eden Hazard, inamtegemea sana mtu mmoja jambo ambalo linaweza kuwashusha kasi ikiwa atashuka kiwango katikati ya msimu ama kuumia ama kutimkia timu nyingine.
“Chelsea wanaweza kuleta ushindani kama wataendelea kumtunza zaidi Hazard ambaye alikuwa na kiwango bora toka alipokuwa kwenye kombe la Dunia, anaweza kuondoka klabuni lakini ni muhimu kwa Chelsea kuhakikisha Hazard anabaki,” Amesema.