Sambaza....

Serikali imewaonya Wanahabari na wadau wa michezo ambao wamekuwa wakiuita Uwanja wa Taifa kwa jina la utani la ‘Kwa Mchina’

Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe katika hafla ya uzinduzi wa nembo maalum itakayotumika kwenye Fainali za Afrika kwa Vijana wenye Umri chini ya miaka 17 (AFCON U17) jijini Dar es Salaam leo.

Dr. Harrison Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe alisema siyo vibaya kwa wadau wa soka kuuita Uwanja wa Taifa kwa majina mengine, lakini kutumia jina la nchi nyingine ni kutoitendea haki Tanzania.

“…..imejitokeza fasheni ya kuita uwanja wa taifa kwa Mchina…. Nawaomba msiuite uwanja huu kwa mchina, uwanja huu hatukupewa zawadi na China, usijenge “concept” kwa watoto kuwa tulipewa zawadi, unaitukana kodi ya Mtanzania”  alisema Dk Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe aliendelea kwa kusema kuwa, Mchina alikuwa ni mkandarasi tu, na wala sio mmiliki wa uwanja wa taifa, na badala yake akapendekeza ni bora kuuita uwanja huo “kwa Mkapa” kama mwanzilishi wa uwanja huo na wala sio “kwa Mchina”.

Mwisho kabisa Waziri Mwakyembe aliwashukuru Wanahabari na  wadau wa michezo nchini, na kudai kuwa, mchango wao ni mkubwa katika maendeleo ya michezo nchini, na kusema kuwa, kukosolewa na wadau hao kumeisadia kamati ya maandalizi ya mashindano ya AFCON U17 kufanya kazi kwa usahihi zaidi.

Sambaza....