Sambaza....

Kuna kipindi yalikuwa ni mazoea, mazoea ambayo yalikera. Ikawa kila siku wao. Vyombo vya habari vilitamani viwaandike wao na wasomaji walitaka wawasome wao.

Wakawa wametengeneza dunia mbili tofauti zenye watu wenye imani tofauti. Dunia ya kwanza ikawa dunia ya Ronaldo yenye imani ya “U-Ronaldo” na dunia ya pili ikawa dunia ya Messi yenye imani ya “U-Messi”.

Kwa pamoja tukakubali kuishi kwenye hizi dunia mbili, tukawa wafuasi wakubwa wa imani za hawa watu wawili (Cristiano Ronaldo na Lionel Messi).

Tuliona ni ngumu kwa mchezo wa mpira wa miguu kukamilika kuitwa mpira wa miguu bila kuwahusisha hawa. Messi na Ronaldo ndiyo walikuwa mpira wa miguu na mpira wa miguu ndiyo ulikuwa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Walibadilishana tu utawala kwa muda wa miaka kumi toka waunyakue kutoka Ricardo Kaka. Ikawa leo akishinda Ronaldo kesho anashinda Messi.

Tukawa tumezoea, tukaona ni jambo la kawaida sana!, nafsi zetu tukaziaminisha kuwa hawa ndiyo wachezaji pekee wanaostahili kushinda kila kitu kila siku.

Ingawa tulitamani sana siku moja aje atokee mmoja ambaye angeikia katikati yao kuvuruga utawala wao. Kila ambaye tulimtabiria hakuweza hata kukaribia eneo ambalo wawili hawa walikuwepo.

Kila tuliyekuwa tunatamani awe mbadala alivuma kwa msimu mmoja tu na msimu mwingine wa pili anapotea, hii ni tofauti na wawili hawa ambao wamedumu kwa muda wa miaka 10 bila kushuka.

Kila mwaka kwao ulikuwa mwaka wa kujivua gamba. Hawakukubali kukaa na gamba kwa muda mrefu sana katika ngozi zao.

Walitamani kuonekana wakiwa wamenawili vizuri na wakiwa wanavutia mbele ya macho ya watu wengi. Kwa kifupi walikilinda kiwango chao cha mpira wa miguu kama ambavyo mwanamke kigoli anavyolinda urembo wake.

Muda mwingi walitumia kwenye kioo kutazama sura ya miguu yao ikoje?, na kila walipokuwa wanatoka kwenye kioo na kuingia uwanjani walikuwa wanafanya vitu ambavyo vilitufanya sisi kujivunia kuwatazama.

Hatujutii macho yetu kumuona Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, wachezaji ambao wameweka rekodi nyingi sana kwenye mpira wetu wa miguu.

Rekodi ambazo ni mlima kwa kizazi kinachokuja kuvunja. Rekodi ambazo ziliwafanya wagawane Ballon D’or katikati kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Ilikuwa ni mazoea ambayo yalipitiliza na kuwa kero!, tulikuwa tunakereka kuwaona wao kila siku, watu ambao hawakuwa wepesi wa kushiba mafanikio yao binafsi.

Ndiyo maana hata Luka Modric aliposhinda tunzo ya FIFA wengi wetu tuliona tumepatiwa ladha mpya, ladha ambayo tulikuwa tunaitamani kwa muda mrefu.

Ndiyo maana tulimwani sana Neymar, tukampa muda kuwa atakuja kuvunja utawala wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Tuliamini kupitia miguu yake kuwa inaweza ikaleta upinzani kwa hawa watu wawili, ila baada ya yeye kupiga teke matamanio yetu kwa pesa za PSG kila kitu kikawa kimeharibika.

Siyo mchezaji ambaye anaweza kufika katika kiwango cha Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Maisha yake ameamua kuyahamishia kutoka uwanjani mpaka kwenye matangazo ya biashara. Akili yake inafikiria pesa tu! na anatumia muda mwingi sana kutengeneza matangazo bora kuliko kufunga magoli bora ambayo yatamwezesha kushinda Ballon D’or.

Taratibu huyu kwa sasa tumeshampoteza, tusubiri tena mpaka siku ambayo atashtuka na kukumbuka kuwa yeye ni mmoja wa watu ambao tulitegemea atengeneze dunia yake ya kwake peke yake kama ambavyo tulivyokuwa tunatamani kwa Eden Hazard pia.

Mchezaji ambaye anauwezo mkubwa sana! , mchezaji ambaye Jose Mourinho aliwahi kusema ni zaidi ya Cristiano Ronaldo lakini kwa bahati mbaya Jose Mourinho alishindwa kumfanya afike mahali ambapo Cristiano Ronaldo alipokuwepo.

Hata Antoine Conte alishindwa hili!, wote wawili (Jose Mourinho na Antoine Conte) muda wote walikuwa wanafikiria namna ya kujizuia hii ni tofauti na Chelsea ya Mauricio Sarri.

Kocha ambaye anamtengeneza Eden Hazard ambaye ndiye tulikuwa tunamtamani sana. Anafunga sana na kutoa pasi za mwisho nyingi sana.

Anaibeba timu yake katika nyakati ngumu kwa uwezo wake binafsi. Kwa kifupi Mauricio Sarri amefanikiwa kumtengeneza Eden Hazard hatari zaidi ambaye ana vigezo vyote vya kuwa mchezaji bora wa dunia , kazi ambayo Antonio Conte na Jose Mourinho walishindwa kuifanya!.

Sambaza....