Kocha wa klabu ya soka ya Chelsea Maurizio Sarri ametoa sababu za kumuanzisha benchi mshambuliaji wa pembeni wa timu hiyo Eden Hazard katika mchezo wa nusu fainali ya Uropa Ligi dhidi ya Eintracht Frankfurt ambapo uliisha kwa sare ya 1-1.
Sarri amesema haikuwa busara kumuanzisha mchezaji ambaye amecheza karibu katika kila mchezo msimu huuna mbali zaidi amecheza kwa dakika zote katika michezo 10 iliyopita hivyo ilikuwa ni kama sehemu ya kumpumzisha mshambuliaji huyo.
“Eden alianzia benchi kwa sababu amecheza michezo 10 mfululizo, sio rahisi kwa mchezaji pia kucheza michezo 70 kati ya 75 kwa msimu mzima, wakati mwingine wanahitajika kupumzika au sio kwa kucheza dakika zote 90,” amemzungumzia Eden ambaye aliingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Willian.
“Tunataka kufika fainali, na sasa ninahitaji kushinda taji, hata ukiangalia miezi mitatu iliyopita tulikuwa kwenye kipindi kigumu lakini sasa tupo kwenye nne bora na pia tupo nusu fainali Uropa, hivyo nadhani tunahadhi ya kuchukua ubingwa huu,” Sarri ambaye timu yake ilipoteza kwenye fainali ya michuano ya ligi dhidi ya Manchester City mapema mwaka huu amesema.
Chelsea walitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo ambao ulipigwa nchini Ujerumani kwenye uwanja wa Commerzbank Arena, ambapo Filip Kostic ndiye aliyeanza kuifungia Frankfurt kabla ya Pedro Rodriguez kusawazisha na kuufanya mchezo wa marudiano kuwa mrahisi kidogo kwa Chelsea ambao watahitaji sare ya bila kufungana ama ushindi wa aina yoyote.