Kiungo wa zamani wa Arsenal na Manchester City Samir Nasri anatarajiwa kufanyiwa vipimo na klabu ya wagonga nyundo wa London West Ham United kwa ajili ya kusajiliwa klabu hapo baada ya kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi 15 sasa.
Imetajwa kwamba kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 ambaye alifungiwa miezi 18 baada ya kukutwa na dawa za kusisimua misuli anaweza kujiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa miezi sita kuanzia Januari 1, 2019 lakini mkataba huo ukiwa na kipengele cha kuongeza.
Samir kabla ya kukumbwa na kadhia hiyo alikuwa akiitumika klabu ya Antalyaspor ya Uturuki na kama atajiunga na West Ham, basi ataungana na kocha wake wa zamani akiwa Manchester City Manuel Pellegrini.
Inasemekana kwamba mwaka 2016 akiwa anaitumikia Sevilla ya Uhispania, Samir alitumia milimita 500 ya dawa iliyokatazwa michezoni (micronutrient) ambayo ilizidi kiwango halisi.